Barabara Bagamoyo-Tanga itakavyoifungua nchi kiuchumi

FEBRUARI 26, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barara ya Bagamoyo (Makurunge) – Pangani kupitia Saadani hadi mkoani Tanga inayojumuisha Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mohamed Besta anasema barabara hiyo ina urefu wa kilomita 256.

Anasema barabara hiyo ni sehemu ya barabara za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayounganisha nchi Kenya na Tanzania kwa ukanda wa Pwani na ipo kwenye ushoroba wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Mji wa Malindi
kupitia miji ya Mombasa na Lungalunga kwa upande wa Kenya na Horohoro, Tanga, Pangani hadi Bagamoyo kwa
upande wa Tanzania.

Besta anaeleza kwamba utekelezaji wa barabara hiyo umegawanyika katika sehemu nne, ya kwanza ikiwa ni ujenzi wa barabara kutoka Pangani hadi Tanga yenye urefu wa kilometa 50 ambao unaendelea na umefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.

Anafafanua, utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza ya mradi ulianza Novemba 15, 2019 na ulipangwa kukamilika Novemba 14, 2021 na kwamba muda umeongezwa kutokana na sababu mbalimbali za kimkataba, na mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni 16, mwaka huu.

Ujenzi wa Daraja la Mto Pangani ukiendelea.

Anasema sehemu ya pili ya mradi ni ujenzi wa Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525 pamoja na Barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 25.6. Ujenzi wa mradi huo wa Daraja unaendelea na unafadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

“Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 52.88. Muda wa mkataba uliokwisha kupita ni miezi 25.83. Hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh 36,638,384,300 wakati Mhandisi Mshauri ameshalipwa Sh 743,516,575,” anaeleza Besta.

Anasema sehemu ya tatu ya mradi ni ujenzi wa Barabara ya kutoka Mkange – Mkwaja – Tungamaa, yenye urefu wa kilometa 95.2, ikijumuisha barabara unganishi ya Kipumbwi yenye urefu wa kilometa 3.7. Kwa mujibu wa Besta,
ujenzi wa mradi huo unaendelea ukifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Anasema kazi hiyo ilianza Aprili Mosi, 2022 na utekelezaji wake umefikia asilimia 45.64 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 88.79. Anaendelea kueleza kuwa Mkandarasi ameomba muda wa nyongeza na Mhandisi Mshauri anaupitia kwa mujibu wa mkataba.

“Sehemu ya pili na ya tatu, mradi unafadhiliwa kwa pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo AfDB imetoa mkopo wa dola milioni 169.98 za Marekani, sawa na Sh Bilioni 390.1, na Serikali ya Tanzania inachangia dola millioni 25.48 sawa na Sh Bilioni 58.47,” anasema.

Anafafanua kuwa, mchango wa serikali kwenye miradi hiyo utatumika kulipia fidia, kodi na tozo katika utekelezaji wa mradi. Besta anasema sehemu ya nne ni ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Mkange yenye kilometa
73.25 ambazo utekelezaji wake unasubiri taratibu za upatikanaji wa fedha.

Baada ya kuweka jiwe la msingi, Rais Samia Suluhu Hassan anaeleza namna barabara hiyo itakavyosaidia mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla katika kuboresha shughuli zinazohusisha barabara hiyo. Rais Samia anasema barabara hiyo itaifungua Tanga kibiashara na kiuchumi na kwamba kupitia barabara hiyo, eneo huru la kiuchumi linakwenda kujengwa ambalo litaihusisha pia Kenya.

“Barabara hii tunayoiunanisha inakwenda kuifungua Tanga kiutalii na kibiashara pia, maeneo kadhaa ya utalii, sehemu mbalimbali za Tanga ambazo hazifikiki kwa barabara hii ni rahisi kumtoa mtalii Saadani na kumpeleka maeneo mengine na kufanya utalii ndani ya Tanga,” anasema Rais Samia.

Anaeleza kuwa mradi huo unaunganisha maeneo mengi kutoka Bagamoyo mpaka Kenya na kuwa kutokana na miundombinu kuwa rahisi serikali itajenga Kongani kubwa la viwanda Bagamoyo.

“Pia tunaiunganisha Tanga tena kupitia Pangani, Pangani hii itaunganisha majimbo mengi ya Bagamoyo na Tanga na itakwenda moja kwa moja mpaka kwenye mpaka wetu na Mombasa ambako Mombasa kule nadhani kwa kupitia mfadhili huyuhuyu na wenyewe wanajenga kuelekea mbele na kutuunganisha na bandari ya Mombasa,” anaeleza.

Anasema barabara hiyo pia itaunganisha Pwani ya Afrika Mashariki kwani baada ya kutoka mpaka wa Horohoro kupita Tanga, Bagamoyo na hadi Dar es Salaam inakuwa rahisi kufika Mtwara na Lindi.

“Naambiwa kwamba Pangani hapa ni wakulima wazuri wa mkonge, mihogo na nazi, sasa hii barabara inakwenda kutafuta biashara na pengine kuwavutia wakulima zaidi wa mihogo kwa sababu mahitaji yatakuwa makubwa soko lipo linafikika litakwenda kuchochea haja ya kuongeza kilimo katika maeneo hayo,” anasema.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akitoa taarifa ya mradi huo

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega anasema barabara hiyo ni miogoni mwa kazi zinazoendelea kutekelezwa na serikali ya Awamu ya Sita na kwamba ujenzi huo utahusisha pia ufungaji wa taa 240. Anasema mji wa Pangani
peke yake utawekwa jumla ya taa 200 na kufikia idadi ya taa 400 zitakazokuwa Pangani kuboresha usalama wa
miundombinu ya Barabara.

Pia, anasema daraja hilo ni mwendelezo wa kazi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga madaraja makubwa ikiwa ni baada ya kukamilika kwa madaraja manane nchini yalioongeza tija katika usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

“Madaraja hayo moja maarufu ni lile la Dar es Salaam la Tanzanite, jingine ni Kitengule la Kagera na la Msingi pale Singida. Haya ni kati ya yale madaraja nane yenye thamani ya Sh bilioni 381, ambayo uliyakuta yakiendelea ukayakamilisha,”anaeleza Ulega.

Pia, anasema Rais Samia alikuta barabara zinaendelea kujengwa na kati ya hizo kilometa 1,366 zimekamilishwa kwa thamani ya Sh trilioni 27 na kwamba jumla ya kilometa 2,031 za barabara zinaendelea kujengwa nchini zikiwemo za Bangamoyo – Mkange – Tungamaa – Pangani na Tanga.

Anaahidi kuwa wizara yake itasimamia usiku na mchana mradi huo bila kuchoka ili ukamilike kwa wakati na wananchi wapate matunda ya maendeleo hayo.

“Wizara ya Ujenzi ikiwa inamdai mkandarasi, inamwambia asicheke wala, afanye kazi usiku na mchana hadi kieleweke, Watanzania waendelee kupata matunda ya uhuru wao,” anasisitiza Ulega.

Meneja Mkazi wa Benki ya Afrika (AfDB) Dk Patricia Leverley, anasema jiwe hilo la msingi lililowekwa la ujenzi wa barabara hiyo linawakilisha ndoto kubwa ya kihistoria ya kuziunganisha nchi za Tanzania na Kenya na kuwa AfDB inaona fahari kushiriki kuitekeleza.

Anasema ili Tanzania ifikie uchumi wa kati inaouhitaji, serikali inahitaji kujenga madaraja ya kisasa zaidi, na viwanja vya ndege vya kisasa.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huu. Ambacho napenda kuwajulisha ni kwamba mradi huu tunaoujenga hapa Tanzania, nia yetu ni kuunganisha bara kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo Misri,” anasema Leverley.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button