Barabara Mianzini-Ngaramtoni kukamilika Septemba

ARUSHA: WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe kumsimamia kikamilifu mkandarasi Stecol Corporation anayejenga barabara ya Mianzini-Ngaramtoni km 18 kuhakikisha inakamilika ifikapo Septemba mwaka huu.

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo, Ulega amesisitiza kufanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa wakati ili kurahisisha usafiri na usafirishaji jijini Arusha.

Amesisitiza ujenzi wa barabara katika miji na majiji uendane na uwekaji taa za barabarani zinazotumia jua ‘solar power’ ili kupendezesha mitaa na kuiwezesha kupitika wakati wote.

“Mh.Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara jijini Arusha hivyo hakikisheni kazi inafanywa kwa ubora, hatutakubali barabara iharibike baada ya muda mfupi ,”amesisitiza Ulega.

Aidha, waziri huyo amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwa serikali itazijenga barabara zote unganishi na wezeshi jijini Arusha ili kupunguza msongamano wa magari na kuendana na maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) 2027.

“Tutahakikisha tunaondoa msongamano kwa kuzijenga barabara zote zenye msongamano na zinazounganisha na kiwanja cha mpira,” amesema Ulega.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Arusha nakusisitiza itachochea ukuaji wa sekta ya utalii  na kukuza uchumi wa watu jijini humo.

Mtendaji Mkuu wa  Tanroads, Mhandisi, Mohamed Besta amesema serikali imetenga Sh bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo na wamejipanga kuhakikisha miradi ya  barabara na madaraja inayoendelea mkoani Arusha inasimamiwa na kukamilika kwa wakati.

Habari Zifananazo

Back to top button