Madiwani waomba utafiti wa mbolea
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi limeiomba serikali kufanya utafiti wa mbolea kwa msimu ujao wa kilimo ili kufahamu endepo unaendana na ardhi ya eneo husika.
Ombi hilo linalenga kutatua changamoto na malalamiko yaliojitokeza kwa wakulima ya kuharibika kwa mazao kutokana na mbolea waliotumia msimu huu.
Hoja hiyo iliibuka kutokana na baadhi ya madiwani kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wao kuhusu kuharibika kwa mazao huku wakidai uharibifu huo umetokana na matumizi ya mbolea kwa msimu huu.
“Sijajua Serikali ina mpango gani wa kudhibiti juu ya uzalishaji wa mbolea, ninaamini watadhibiti wazalishaji wa mbolea lakini je wamefanya utafiti juu ya usafirishaji wa mbolea?
” Amehoji Elias Fyula Diwani wa Kata ya Mtapenda
Akijibu hoja hizo Afisa kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Nsimbo Daniel Walakunga amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo kuhusu utendaji mbovu wa mbolea kwa msimu huu.
“Ni kweli malalamiko yalitokea sana kuhusiana na utendaji mbovu wa mbolea hii, nasisi tulijaribu kuwasiliana na wenzetu walikuja ofisini hapa,wao walisema inawezekana kwenye aina ya matumizi kidogo ndio palikuwa pana shida miongoni mwa watu, tukawaambia sasa hii kitu itatuletea shida, kama nyinyi mlileta tuu mbolea sokoni halafu hamkutoa namna ya matumizi” amesema Walakunga
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Gilbert Bayaga amesema tayari suala hilo limefika katika ngazi ya mkoa na limewasilishwa wizarani kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi.
Aidha amewataka watanzania kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupatikana kwa watu waliohusika na uchakachuaji wa mbolea na kusababisha hasara kwa wakulima.