MSEMAJI wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalam wa ndani kushirikiana na wataalam kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi kuhusu ajali ya Ndege ya Precision Air ya Novemba 6, 2022 ili kupata chanzo cha ajali na mapendekezo ya hatua zitakazochukuliwa.
Akizungumza leo Novemba 14, 2022, Msigwa amesema baraza hilo limetoa maelekezo hayo kwa kuzingatia kuwa Tanzania imetiliana saini katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mara baada ya ajali ya anga kutokea.
“Baraza limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe kwa namna mbalimbali ambazo zitatuwezesha sisi kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulionao sasa katika kukabiliana na majanga pale yanapotokea…
…Na tutamaliza na ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea, hatua hizi zote tayari zimeshaanza.”ameongeza Msigwa.
Msigwa ametaja hatua tatu zinazofanyika katika uchunguzi ikiwemo timu ya uchunguzi ya ajali ya ndege ambayo inafanya uchunguzi wake na kutoa maelezo ya awali ndani ya siku 14, inafuatiwa na ripoti ya awali ambayo inatolewa ndani ya siku 30.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi huu unafanyika na baada ya uchunguzi kukamilika watajulishwa. Aidha, Baraza linawashukuru na kuwapongeza wote waliohusika katika uokozi baada ya ajali hii kutokea.
Maeneo ya uchunguzi yote yanaainishwa na timu za wachunguzi, taratibu zote za kimataifa ambazo zinaelekeza juu ya maeneo yanayopaswa kufanyiwa uchunguzi zinazingatiwa.