HALMASHAURI ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, imekamilisha ujenzi wa Vyumba 14 vya Madarasa vyenye thamani ya Sh280 milioni, vitakavyoweza kuchukua zaidi ya Wanafunzi 700 wapya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. Khalid Mbwana ameeleza hayo Jana na kusema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto ya uhaba wa Vyumba vya Madarasa hasa wakati wa udahili wa Wanafunzi wapya wa Kidato cha Kwanza na wengine wanaoendelea na masomo katika Shule za Msingi na Sekondari Mkoani humo.
Akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi hiyo wakati wa Mahojiano Maalum na Meandishi wetu, Bw. Mbwana alisema kuwa ujenzi wa Madarasa hayo unafanyika katika Shule za Vijijini na Mijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
“Ujenzi wa Vyumba hivyo 14 vya Madarasa utasaidia wanafunzi 700 kudahiliwa Kwa Muhula ujao was Masomo mara baada ya Matokeo ya Wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza 2023 yatakapotolewa,” alisema.
Kwa upande mwingine akizungumzia baadhi ya taarifa zilizosema kuna baadhi ya wanafunzi wameahirisha Masomo au kushindwa kuendelea na Masomo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, Bw. Mbwana alisema hakuna taarifa rasmi wala ushahidi unaoonyesha kuwa kuna ni Wanafunzi waliolazimika kuacha au kushindwa kuendelea na masomo kutokana na uhaba wa Vyumba vya Madarasa.
“Sisi Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi hatuna ushahidi kuwa wapo wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwani kila Mwaka Serikali na Jumuiya za Wazazi kwa kushirikiana hujenga vyumba vya madarasa vya kutosha kudahili wanafunzi hao,” alisema.
Kwa upande mwingine akizungumzia ufaulu wa wanafunzi katika Wilaya hiyo Bw. Mbwana alisema ni matarajio yao kuwa asilimia 100 ya watahiniwa 6,112 waliofanya Mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba kwa mwaka huu watafaulu kwa mujibu wa Sera ya Elimu ambapo malengo ni kwa wanafunzi wote kufaulu.
“Kwa hiyo, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi za ujenzi wa vyumba vya madarasa, imesaidia wananchi kuwapunguzia adha, ambapo awali kabla ujenzi wa Vyumba vya Madarasa unaanza, ulikuwa unatupa matatizo kuhusu ukosefu wa vyumba vya madarasa ili kupokea idadi kubwa ya wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo,” aliongeza.