Baridi yaathiri afya, uchumi Njombe

HALI ya baridi imeathiri afya na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Njombe.

Baridi katika mkoa huo inaongeza magonjwa yanayohusiana na mazingira ya baridi na imeathiri baadhi ya biashara ikiwemo ya bodaboda

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Dk Jagadi Ntugwa alisema kipindi cha baridi husababisha kupungua kwa kiwango cha unywaji wa maji hivyo kuchangia ongezeko la magonjwa yakiwemo ya mawe kwenye figo kutokana na upungufu wa maji mwilini.

“Katika kipindi hiki, watu hupungukiwa na kiu, hivyo hawanywi maji ya kutosha, hali inayosababisha figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo,” alisema Dk Ntugwa.

Katika maeneo mengi ya Njombe, familia hutumia moto wa mkaa ndani ya nyumba ili kujikinga na baridi.

Kufanya hivyo kunatajwa kuwa na madhara kwa afya ya binadamu hasa watoto na wazee ambao hupatwa na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Pia, moshi unaotokana na majiko ya mkaa hayo, huongeza uwezekano wa kupata kikohozi sugu, pumu na maambukizi ya mapafu.

“Ndiyo tunaelewa si salama, lakini hakuna jinsi. Baridi ni kali mno na tunajitahidi kutoa majiko nje kabla ya kulala,” alisema mkazi wa Njombe, Dora Deule.

Katika sekta ya usafirishaji, madereva wa bodaboda wanadai baridi kali imepunguza idadi ya abiria wanaotumia usafiri huo na kwamba wananchi wengi wanasafiri kwa pikipiki za miguu mitatu (bajaji) kuepuka baridi.

“Muda huu wa baridi tumebaki vijiweni, watu wanapendelea kupanda bajaji kwa sababu hazipigi baridi. Kazi imekuwa ngumu,” alidai dereva wa bodaboda, Onesmo Ng’ang’ane.

Baadhi ya wakazi wa Njombe wanadai baridi imeongeza gharama za maisha kwa sababu miili inahitaji joto zaidi hivyo hulazimika kula mara nyingi zaidi kuliko kawaida.

“Tunalazimika kula zaidi ili kupata joto. Chakula kinahitajika mara nyingi zaidi na hii inaongeza gharama kwa familia,” alisema Michael Mwamlima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button