Barrick yaja na kombe la mahusiano

Barrick yaja na kombe la mahusiano

MGODI wa dhahabu wa Barrick North Mara, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, umeandaa mashindano ya soka ya kuwania kombe la mahusiano yaliyozinduliwa juzi.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema kwenye uzinduzi wa mashindano hayo kuwa, mashindano hayo yanashirikisha timu kutoka vijiji 16 vinavyozunguka mgodi huo na yalizinduliwa rasmi juzi katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe wilayani Tarime.

Mashindano haya yenye kaulimbiu ya “Mahusiano bora kwa uwekezaji endelevu”, uzinduzi wake ulishirikisha wananchi kutoka vijiji mbalimbali na wafanyakazi wa Barrick North Mara, ambapo waliburudika kwakucheza  michezo ya aina mbalimbali na kushuhudia mechi kati ya timu ya Kewanja na Mosege.

Advertisement

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mtenjele, aliyeongozana na viongozi mbalimbali wa serikali wilayani humo.

Vijiji ambavyo timu zake zinashiriki katika mashindano hayo ni Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwanga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichume, Mji Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangoro na Nyarwana.

Lyambiko, alisema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga na kudumisha uhusiano katika jamii.

“Bila mahusiano bora na jamii inayotuzunguka sisi kama kampuni hatuwezi kufanya kazi kwa utulivu, hali ambayo inaweza kusababisha uwekezaji wetu usilete manufaa katika pande zote mbili,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Mntenjele, aliwataka washiriki wa mashindano hayo kucheza kwa amani na wasimamizi husika kutenda haki bila kupendelea timu yoyote.

Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliipongeza Barrick North Mara, kwa kuandaa mashindano hayo akisema yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi huo ili kuwezesha kila upande kunufaika.