Bashungwa awaondoa hofu watumia vivuko Dar

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni-Magogoni, juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.

Moja ya Kivuko cha Kigambini

Ameyasema hayo leo Mei 28, 2024 wakati alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.

“Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na Kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunao fahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki,” amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa, sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwaajili ya kupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.

SOMA: ‘Wazee wasilipe nauli kwenye pantoni’

Pia, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutaweka machaguo kwa abiria ambapo watakuwa na chaguo. Ukitaka kutumia kivuko cha TEMESA sawa au ukitaka cha AZAM muda mchache kuvuka kwasababu zile ni ndogo siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amesema Wizara inatambua changamoto ya wananchi ni huduma bora ya vivuko na kusema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu wataanza kutekeleza mpango huo utakaotoa wigo kwa wananchi kuchagua huduma wanayotaka kutumia.

“Wapo wanaotaka kushinikiza ili utaratibu na mwelekeo uende kama wanavyotaka wao, sisi hatuendi hivyo,” amesema Bashungwa huku akisema kuwataja watu hao ni kuwapa sifa.

Mnamo Novemba 11, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Kigamboni, alithibitisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam mesema itaingia mkataba na sekta binafsi kwa ajili ya uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi,

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kigamboni, Rais Samia amesema kwa sasa kuna kivuko kidogo cha mtu binafsi kinachosaidia kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Kigamboni baada ya vivuko vikubwa kupata hitirafu.

“Tunatambua kuna kivuko kinafanyiwa matengenezo. Vilevile kuna kivuko kipya kinajengwa na kitakapofika tutaingia mkataba na sekta binafsi ili kukuindesha,” amesema Rais Samia.

Wakazi wa Kigamboni wamekuwa wakilalamikia huduma duni za kivuko kutokana na changamoto za matengenezo ya mara kwa mara na wakati mwingine huduma mbovu. Mbunge wa Kigambani Dk. Faustine Ndugulile amemwambia Rais Samia wananchi wa Kigamboni baado wanateseka na dosari za kila siku za uendeshaji wa kivuko hicho.

“Tunaomba kama inawezekana kivuko hicho kikabodhiwe kwa sekta binafsi,” alishauri Dk Ndugulile.

Rais Samia amekiri kuwa uendeshaji wa kivuko hicho ni mzigo kwa serikali na kwamba kivuko hicho kikiwa chini ya usimamizi wa sekta binafsi kitapunguza mzigo kwa serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button