Batuli: Serikali ina deni kudhibiti wadukuzi kazi za sanaa

DAR ES SALAAM: SERIKALI ina deni la kuhakikisha inaweka mfumo bora wa kudhibiti wadukuzi wa kazi za sanaa ili kuwahusika wa kazi hizo waweze kufaidika lakini kutopoteza mapato.

Kauli hiyo imetolewa na mwigizaji mkubwa wa filamu nchini, Yobnesh Yusuph maarufu ‘Batuli’ alipozugumza na HabariLEO kuhusu mwenendo wa kiwanda cha filamu nchini.

Akizungumza leo Juni 4, 2024 na mwandishi wa mtandao huu, Batuli ambaye kwa sasa ana miaka 24 katika sanaa hiyo amesema endapo serikali itadhibiti biashara hiyo haramu itaongeza mauzo halisi na halali kupitia kazi zao, lakini pia serikali iwasaidie kusaka masoko ya nje.

Advertisement

“Bahati mbaya viongozi husika wamekuwa wakibadilishwa mara kwa mara naamini isingekuwa mabadiliko ya uongozi kwa mtindo huo tungefika mbali sana, tulianza kuyaona wakati wa Mheshimiwa Nnape Nauye na pia kwa Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa, nakiri walitusogeza pakubwa sana,” amesema Batuli.

Batuli ametaja changamoto zinazowakabili waigizaji kuwa ni uwepo wa malipo madogo tofauti na ukubwa wa kazi wanazofanya, ambapo mwigizaji akikataa kutokana na hilo, mwingine anakubali amesema hali hiyo inashusha thamani ya kazi yao.

“Changamoto nyingine ni kutokuwa na sheria na kanuni sahihi za kuigiza waigizaji wapya hawapitii madarasa ambayo sisi tulipitia, wengi wao wanatoka waliopotoka na umaarufu wa vituko vyao vya hovyo, mitandaoni kisha wanajazwa kwenye uigizaji matokeo yake ni kuwa na waigizaji wenye skendo chafu na vituko vya ajabu,” ameeleza Batuli.

Batuli amesema kwa hali hiyo wakati mwingine inakuwa ngumu mzazi kumruhusu mtoto ambaye ana kipaji na elimu ya sanaa ya uigizaji kuingia kwenye kazi hiyo.

Pia amegusia suala la mazingira ya kufanyia kazi zao, ambapo amesema hakuna maeneo maalum yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kazi zao za uigizaji.

Batuli amegusia ubora wa kazi za sasa na kipindi cha nyuma ambapo ameeleza zamani kazi zilifanywa kwa ushindani wa hali ya juu, wakikuwa wakichuana kwa kuangalia zaidi soko tofauti na sasa hivi, ambapo kutokana na sababu hiyo rasmi wakongwe wameamua kurudi kazini na kwamba watu wategemee vita ya kazi kutoka kwao.

Mwigizaji huyo ameeleza suala baadhi ya watendaji wa filamu kuwa na majukumu mengi kwa wakati mmoja, ambapo amesema miaka ya nyuma suala hilo lilitokana na kutokuwa na watu wengi ila kwasasa wasomi wako wengi ambao wamejikita katika uongozaji wa filamu.

“Mbaya zaidi sisi hatuna wenye ujui wa teknolojia ya hali ya juu, watu wenye ujuzi wa teknolojia ya hali ya juu, wenzetu mataifa yaliyoendelea wanatumia sana, sisi tunatumia sana kipaji na uhalisia,” ameongeza Batuli.