BENKI ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (UDSM-CoICT) zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo matano ikiwemo kufanya utafiti wa matumizi ya akili mnemba (AI) na athari zake katika tasnia ya fedha.
Eneo lingine ni ukuzaji wa ubunifu kwa matumizi ya teknolojia ili kuendeleza ushindani katika sekta ya kifedha ambayo inakua kwa kasi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo leo Dar es Salaam, Ofisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay amesema kuwa mkataba huo utachangia kuchochea ubunifu na kuwezesha utatuzi wa changamoto zinazozunguka jamii na taifa kwa jumla.
‘’Kuhusu utafiti wa teknolojia na maarifa benki ya NMB na CoICT watashirikiana pamoja katika kufanya utafiti wa teknolojia na kuchunguza athari za matumizi ya akili mnemba katika tasnia ya fedha,’’ amefafanua.
Amesema kuwa maeneo mengine ya mkataba huo ni ukuzaji wa vipaji na ujuzi kati ya NMB na Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) ambako watashirikana katika kutambua na kuendeleza vipaji kupitia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika nyanja ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
‘’Pande zote zitashirikiana katika kutoa fursa kwa wanafunzi kujaribu teknolojia tofauti zinazoweza kuwa na athari chanya katika sekta ya kifedha ikiwemo kujaribu nadharia zao za kibunifu kupitia mfumo wa NMB Sandbox,’’ amesema Akonaay.
Ameeleza kuwa eneo lingine ni mageuzi ya kidigitali, pande hizo wataendelea kuwekeza kwenye mageuzi ya kidijitali ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuboresha huduma kwa wateja.
Taasisi hizo zitafanya kazi katika kuandaa wataalam na rasilimali watu ambayo itasaidia kuongeza kasi ya mabadiliko ya kidijitali na kuongeza tija.
Pia makubaliano hayo yanahusisha msaada wa kifedha wa masomo kusaidia program za kibunifu pale itakapoombwa na chuo hicho na uidhinishwaji wa ndani utafanywa na benki hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema kuwa wanatamani matumizi ya akili mnemba yaweze kutambua lugha mbalimbali za Tanzania kwamba kwa kufanya hivyo, utawezesha utoaji huduma.
Amesema kuwa kuna programu mbalimbali za akili mnemba kama vile Gemini, Chart GPT lakini hazitumii lugha za asili za Tanzania hivyo, kwa kutumia utafiti wataona namna ya kuwezesha lugha za Tanzania zitumike kuwafikia walengwa.
Pia amesema ‘’Tunao vijana wazuri kwenye ubunifu tutawatengeneza waweze kuendesha uchumi kwa kufungua kampuni na biashara na sio kuajiriwa tu.”