Benki yaunga mkono jitihada za Rais upandaji miti

PWANI: “Upandaji wa miti kwa wingi pamoja na mikoko kutasaidia kurudisha hali asilia ya bahari na kupunguza kasi ya mmomonyoko wa ardhi,” alisema Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Januari 27, 2024 katika siku yake ya kuzaliwa.

Katika siku hiyo, Rais Samia na wananchi wengine walipanda miti 4720 eneo la Donge Muwanda jimbo la Tumbatu.

Katika kuendelea jitihada hizo, Benki ya Standard Chartered imepanda miche ya miti 2000 katika Shule ya Msingi Fukayosi iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

SOMA ZAIDI: Samia aadhimisha siku ya kuzaliwa kwa namna hii

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhamasisha ulinzi wa mazingira.


Akizungumza katika zoezi la upandaji miti kwenye shule hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu Standard Chartered Herman Kasekende, amesema zoezi hilo wanalolifanya ni muhimu kwani litasaidia kupunguza hewa ukaa ambayo ni sumu mbaya.

“Wanasayansi wamefanya tafiti mbalimbali ambapo wanasema mti mkubwa una uwezo wa kufyonza karibu kilo 21.77 mpaka kilo 31.5 za hewa ukaa kwa mwaka, hivyo kuna umuhimu mkubwa tukaongeza jitihada za upandaji miti katika maeneo yetu”amesema.


Amesema katika benki yao wameweka mpango ambao umelenga ifikapo mwaka 2050 kufikia neti 0 (kupunguza hewa ukaa) kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Majid Mhina amesema kiwango cha uzalishaji wa hewa ukaa ni kikubwa kuliko idadi ya miti, jambo linalochangia kuongezeka kwa magonjwa na uhaba wa chakula.

Mhina amewasihi wadau kuongeza juhudi za upandaji miti kwa ajili ya kurejesha mvua na kuongeza uzalishaji wa chakula.

Pamoja na hayo, Mhina ameipongeza Standard Chartered kwa kujitolea kwake bila kuyumba kwenye uendelevu wa mazingira kupitia mpango wake wa upandaji miti, ikisisitiza upatanisho na malengo ya kitaifa ya hatua za hali ya hewa.

“Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayogusa uchumi, afya, na maisha ya wananchi wetu. Mipango kama hii siyo tu kwamba inarejesha uoto wa asili, bali pia inawafundisha vijana wetu umuhimu wa utunzaji wa mazingira,”amesema.

Amesema kwa ushirikiano baina ya serikali, sekta binafsi, na wananchi, wanaweza kufikia lengo la kitaifa la kupanda miti milioni 1.5 katika kila kata huku akisema uongozi wa benki hiyo katika suala hili ni mfano wa kuigwa katika uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.

Benki hiyo imefanya zoezi hilo katika shule ya msingi Fukayosi ambapo imekusudia kuwaandaa wanafunzi kudumisha usawa wa kiikolojia wa muda mrefu na kuongeza ufahamu wa mazingira kwa watoto, waalimu,na wanajamii ili kushiriki katika kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan SDG 13 kuhusu hali ya hewa na SDG 15 juu ya maisha ardhini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button