WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imesema upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi mkoani Kilimanjaro unatarajiwa kukamilika Novemba mwakani ili kuwezesha ndege binafsi na za biashara zenye uwezo wa kubeba abiria 40 zitue na kuruka kiwanjani hapo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema baada ya kuoneshwa filamu ya Royal Tour kumekuwa na ongezeko la watalii nchini hivyo dhamira ya serikali ni kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili kutokwamisha matokeo ya filamu hiyo.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilieleza kuwa Mwakibete alisema hayo mkoani humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi huo.
Filamu hiyo imekuwa na mvuto kwa sababu kuonesha uzuri wa Tanzania vikiwamo vivutio vya utalii na Rais Samia Suluhu Hassan ni mhusika mkuu katika filamu.
Aliziagiza Taasisi za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) zimsimamie mkandarasi anayeboresha kiwanja hicho ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango.
Mwakibete aliuagiza uongozi wa TAA, Tanroads na mkoa wakae kumaliza changamoto zilizopo ikiwamo uvamizi wa eneo la kiwanja ili kutomchelewesha mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando alisema upanuzi wa kiwanja hicho unatumia fedha za ndani zaidi Sh bilioni 12 na tayari mkandarasi kampuni ya Watanzania, Rocktronic Limited ameanza kazi za awali za upanuzi na mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 12.
Motta alisema upanuzi huo utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, barabara za usalama kiwanjani hapo kwa kiwango cha lami na uzio.
Meneja wa kiwanja hicho, Yusufu Sood alisema kwa sasa kiwanja hicho kinahudumia ndege ndogo ambazo si za ratiba zinazoweza kubeba abiria wasiozidi saba na helikopta za watu binafsi hivyo kukamilika kwa maboresho hayo kutaongeza miruko ya ndege na idadi ya abiria.
Utekelezaji wa mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) unaobainisha kuwa ununuzi wa ndege mpya unaenda pamoja na ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya mikoa na vya kimataifa.