Bil 120/- mradi wa HEET zaineemesha MUHAS

CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kimesema kimepata Sh bilioni 120 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS, Dk Harrison Mwakyembe amesema hayo wakati Mahafali ya 19 ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Dk Mwakyembe amesema fedha hizo zimetokana na mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Dunia, na sehemu kubwa zinatumika uendelezaji wa Kampasi ya Mloganzila ikiwemo ujenzi wa Ndaki ya Tiba na kuanzishwa kwa kampasi mpya mkoani Kigoma. “Moja ya faida kubwa ya mradi wa HEET kwa MUHAS ni upanuzi wa wigo wa udahili wa wanafunzi katika fani za afya unaotokana na ujenzi wa miundombinu mipya na ya kisasa kupitia mradi huu,” alisema Dk Mwakyembe.

Ameongeza kuwa kutokana na uhaba wa miundombinu, katika kila wanafunzi 31 wenye sifa kamili za kusoma MUHAS, ni mwanafunzi mmoja tu ndiye anayepata nafasi. Hatahivyo ametolea mfano, katika mwaka wa masomo 2025/2026 kati ya waombaji 31,026 waliokuwa na sifa, ni wanafunzi 986 yaani asilimia tatu ya waombaji wenye sifa kamili ndio waliochaguliwa katika kozi mbalimbali za shahada ya awali.

“Kupitia mradi wa HEET, tutaongeza uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya mara mbili. MUHAS imeendelea kuwa taasisi ya rejea katika utoaji wa ushauri wa kisera kwa serikali na wadau wa maendeleo hasa sekta za afya, elimu ya juu, tafiti na sayansi shirikishi,” alieleza Dk Mwakyembe.

Amesema baraza la chuo limeendelea kusimamia dira ya maendeleo ya MUHAS kwa ukaribu kuhakikisha taasisi zinafuata misingi ya utawala bora, uwajibikaji na usawa wa kijinsia na matumizi ya teknolojia ya usimamizi wa taaluma, tafiti, fedha na rasilimali watu.

“Katika mwaka huu wa 2025, MUHAS imeendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa viwango vya kimataifa kwa kuanzishwa mitaala mipya 14 ya shahada ya kwanza na ya uzamili ili kujibu mahitaji ya sasa ya kitaifa na kimataifa katika sekta ya afya,” aliongeza. SOMA: Prof. Kamuhabwa: Mradi wa HEET umeleta mageuzi MUHAS

Amefafanua kuwa lengo ni kuzalisha wataalamu wa kitaifa wabobezi wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira la karne ya 21. Mbali na hayo, pia programu 11 za uzamili na za ubobezi zilizoanzishwa zinatarajiwa kutoa wataalamu bobezi watakaosaidia kutoa huduma za kibingwa nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, Dk Mwakyembe alisema tafiti za MUHAS zimekuwa chachu ya mabadiliko, sera na huduma za afya nchini, na matokeo yake yamechangia kuandaa miongozo ya kitaifa, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, afya mazingira na sera asilia.

Ametaja baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo ni ukosefu wa vyanzo vya mapato vitakavyokiwezesha kugharamia mambo yake bila kutegemea ruzuku serikalini. Amesema baraza la chuo limeidhinisha kuanzishwa kwa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara kitakachokuwa chini ya makamu mkuu wa chuo kikihusika kujenga ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Appolinary Kamuhabwa alisema katika mahafali ya mwaka huu, chuo kina wahitimu 1,362 ambao kati yao, wahitimu 504 sawa na asilimia 37 ni wa kike wakimaliza katika ngazi za stashahada, shahada za kwanza, uzamili ubobevu na uzamivu.

Amesema wahitimu 108 wametunukiwa shahada na stashahada ya juu katika fani mbalimbali wakati wahitimu 680 watapata shahada ya kwanza na wengine 511 shahada ya uzamili. Sambamba na hao, alisema wahitimu 54 wametunukiwa shahada za uzamili za ubobezi na wahitimu tisa shahada za uzamivu wa udaktari wa falsafa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button