Bil 14.8/- kuboresha Chuo Kikuu Mkwawa

CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimepata zaidi ya Sh Bilioni 14.8 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), zitakazotumika kujenga majengo manne mapya ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha mazingira ya elimu, utafiti na ubunifu vyuoni.

Majengo haya mapya ni pamoja na hosteli ya wanafunzi, maabara ya fizikia, jengo la sayansi, na jengo la media anuwai na elimu maalum ambayo kwa pamoja yatasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi, kuboresha mbinu za ufundishaji, na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Mikataba ya ujenzi wa majengo hayo imesainiwa kati ya chuo hicho na kampuni ya mkandarasi mzawa, Dimetoclasa Real Hope Limited and Mponera Construction.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba hiyo, Kaimu Rasi wa Chuo, Profesa Deusdedit Rwehumbiza alisema mradi huo utasaidia kuwajengea wanafunzi na wahitimu ujuzi na maarifa yanayohitajika kwenye soko la ajira na kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi, jamii na Taifa.

Profesa Rwehumbiza alisisitiza umuhimu wa majengo haya katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kutoa fursa bora zaidi kwa wanafunzi wa kike, ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi wanapoishi nje ya hosteli.

“Mradi huu utaongeza usalama wa wanafunzi, hasa wa kike, na kupunguza matukio ya ukatili na wizi katika hosteli wanazopanga nje ya chuo,” alisema Profesa Rwehumbiza.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, alisema mradi wa HEET, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha elimu ya juu na maendeleo ya viwanda nchini.

Aliwahimiza wakandarasi kumaliza ujenzi kwa wakati na kwa viwango vya juu, akisema, “Tunahitaji uzalendo na uadilifu katika ujenzi wa mradi huu unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15.”

Alisema mradi huo utakisaidia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na matawi yake yote, ikiwemo MUCE, katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji, kujifunza, na kufanya tafiti mbalimbali.

Wanafunzi wa MUCE wameipongeza serikali kwa jitihada hizi, wakionyesha matumaini kwamba ujenzi wa hosteli mpya utapunguza changamoto za malazi na gharama kubwa, ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwao.

Makamu wa Rais wa Chuo hicho, Remisha Gastoni Milazi, alisema kuwa ujenzi huu utaleta mabadiliko makubwa, hususan katika kupunguza changamoto za usalama kwa wanafunzi wa kike.

Rais wa chuo, Steaven Thomas Mgala, alibainisha kuwa hosteli mpya zitaongeza kiwango cha ufaulu kwa kuwa wanafunzi wengi wataweza kujifunza katika mazingira bora na salama.

“Kupatikana kwa hosteli mpya kutaboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza tija katika masomo,” alisema.

Mkandarasi Dickson Mwipopo aliahidi kukamilisha mradi huu kwa wakati na viwango vilivyokubaliwa, akisisitiza umuhimu wa kutumia wakandarasi wa ndani ili kuimarisha uchumi wa taifa na kutoa ajira kwa vijana.

Ujenzi wa majengo haya mapya ni hatua kubwa kwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya elimu na viwanda nchini Tanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button