SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano imesema imefanikiwa kupata mkopo kutoka Benki ya Dunia wa Sh bilioni 19 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuboresha huduma za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Sayansi ya Bahari iliyopo Buyu, Unguja.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu ya Sayansi na Teknolojia, Omar Juma Kipanga wakati akizungumza katika mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Taasisi ya Sayansi ya Bahari yaliyofanyika Buyu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema fedha za mkopo huo zitatumika katika kuimarisha baadhi ya majengo yaliyopo katika chuo hicho kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake na kuanza kutoa huduma.
Aidha, alisema sehemu ya fedha hizo zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kujenga maabara ya kufanya kazi za utafiti wa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika taasisi hiyo.
Aidha, aliipongeza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa kufanikisha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi ya Bahari ambapo katika mwaka 2021 walipatiwa mikopo ya Sh bilioni 467 na kuongezeka hadi kufikia Sh bilioni 570 katika mwaka 2022.
Mapema Kipanga aliwataka wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika taasisi ya sayansi ya bahari ili kwenda sambamba na mikakati na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuingia katika uchumi wa buluu.
Alisema chuo hicho kwa mara ya kwanza kimefanikiwa kutoa jumla ya wahitimu 27 wa shahada ya kwanza katika masuala ya sayansi ya bahari.