SERIKALI kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) itatumia Sh bilioni 2.1 kufikisha umeme wa jua katika visiwa vya Ziwa Victoria vilivyopo Wilaya ya Bukoba na Muleba ikiwa ni mpango maalumu wa kuwawezesha mwananchi kupata huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa (REA) Mhandisi, Hassan Said aliongozana na Mwenyekiti wa Bodi (REA) kuwasha umeme ambao tayari umefika katika kisiwa cha Musira kilichopo kata Miembeni Wilaya ya Bukoba na kuzungumza na mwananchi .
“Ni kweli kuwa Watanzania wanaoishi hapa kisiwani Musira wamekuwa wakifata huduma za umeme mjini hawawezi kufungua biashara kwa sababu hawana umeme lakini serikali imefikisha umeme wa jua kwa punguzo kubwa sana na wao wanachangia kidogo sana hii ni kwa sababu serikali inataka kila mtanzania kutumia umeme bila kujali changamoto za eneo alilopo,”amesema Saidi.
Amesema serikali imedhamiria kuhakikisha visiwa vyote ambavyo havijafikiwa na Gridi ya Umeme wa Taifa unapata umeme kwa chanzo kinachoweza kutoa umeme huku gharama ya asilimia 55 hadi 75 ikibebwa na serikali kulingana na ukubwa wa huduma inayotolewa kwa wananchi na wafanyabiashara walioko visiwani.
Mkurugenzi wa teknolojia za nishati jadidifu na mbadala kutoka REA , Dvera Mwijage amesema kuwa mikoa 7 ya Tanzania, wilaya 16 na kata 43 pamoja na visiwa 118 nchini vitanufaika na umeme jua kwa gharama ya Sh bilioni 8.
Amesema katika umeme ambao umefungwa katika kisiwa Cha Musira kaya 192 zinatarajia kunufaika huku kaya 50 tayari zimeishaanza kutumia mfumo huo,na maeneo yanayotoa huduma za umma kama shule ,Makanisa tayari nao wameanza kutumia mfumo huo.
“Natoa wito kwa wakandarasi ambao watapata kazi katika utekelezaji wa mradi huu kutojihusisha na vitendo vya Rushwa kwa sababu serikali imebainisha mahitaji ya wananchi na kuzingatia maombi yao hivyo wananchi ambao hawajapata kwa hawamu hii watapata hawamu ijayo wakandarasi epukeni Rushwa,”amesema Mwijage
Mwenyekiti wa Bodi ya REA Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alitoa wito kwa wanachi kuchangamkia fursa ya kuunganisha umeme katika makazi yao na maeneo ya biashara Ili kukuza uchumi wao.
Aidha aliwataka kutohujumu miundombinu ya umeme huo kwani serikali imetumia gharama kubwa huku akidai kuwa bodi imerudhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa chachu ya mafanikio kwa wananchi wengi wanaoishi katika kisiwa cha Musira.
Baadhi ya wananchi ambao tayari wameanza kunufaika na mpango huo wa serikali wa kuwafungia nishati ya umeme wa jua, licha ya kuishukuru serikali walielezea matarajio na tija waliyopata baada ya kufungiwa.
Stela Petro ni miongoni mwa wanufaika wa mpango huo, alisema kabla ya kufikiwa na mradi huo alikuwa akivuka ng’ambo ya pili kuongeza umeme kwenye simu, alikuwa akifunga biashara yake mapema ata kuamka kufungua biashara yake mapema ililiwa ngumu.
“Baada ya kufungiwa umeme niweza kuchaji simu kwangu,tunaweza kuchaji taa zetu zinazotumika katika uvuvi kirahisi kuliko olivyokuwa nyuma na anaweza kufanyabiashara zake za kuuza vinywaji na chakula mpaka usiku wakati alikuwa akifunga saa 12 jioni hivyo nimeongeza wateja na kipatao kuongezeka kutoka Sh 30,000 hadi 60,000 kwa siku”amesema Stela.