Bil 27/- msaada kutoka Japan kuboresha afya nchini

Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), zimetiliana saini mkataba wa msaada wa shilingi bilioni 27.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya nchini.
Taarifa ya Wizara ya Fedha imesema mkataba huo umesainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yoichi Mikami na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Hitoshi Ara, kwa niaba ya Serikali ya Japan.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Mwamba amesema fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa-tiba ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.

Dk Mwamba amesema ufadhili huo muhimu unaendana na Mpango wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao pamoja na masuala mengine, unalenga kutatua changamoto za ubora katika utoaji huduma za afya nchini.
“Ufadhili huu unaunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya afya, zinazolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati kwenye jamii,” amesema Dk Mwamba.
Ameongeza kuwa mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Afya na utaboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya hususani Huduma ya Mama na Mtoto kwa kuwa na vifaa-tiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu katika Hospitali saba za Rufaa.
Hospitali hizo niDodoma, Tumbi iliyoko mkoa wa Pwani, Mount Meru iliyoko Arusha, Sekou-Toure iliyoko Mwanza, Songea iliyoko Ruvuma, Maweni iliyoko mkoani Kigoma na Hospitali ya Lumumba iliyoko Zanzibar.
“Msaada huu ni mwendelezo wa ushirikiano unaokua kati ya nchi zetu mbili kama inavyodhihirishwa na kuongezeka kwa idadi ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia misaada na mikopo nafuu,” amesema.
Dk Mwamba ameishukuru Japan kwa ufadhili huo na mingine ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

“Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kwa faida ya watu wetu na Serikali itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” amesema Dk Mwamba.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini, Yoichi Mikami, amesema kwa kutambua ushirikiano wa nchi hizo mbili, Japan imekuwa ikitoa misaada katika sekta ya afya ili kuchochea maendeleo ya watanzania.
“Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Mikami.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Hitoshi Ara, amesema (JICA) imekuwa ikitoa msaada mkubwa katika sekta ya afya ya Tanzania kwa miaka mingi, katika kuimarisha usimamizi wa hospitali na kujenga uwezo wa usimamizi wa ubora wa huduma za afya kupitia mbinu mbalimbali, katika Hospitali za Rufaa za Kanda.
Ara amesema JICA imekuwa ikishuhudia maboresho katika ufanisi, usalama, na ubora wa huduma na wanamini kuwa hayo yote yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia lengo la Mpango was Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Wote (Universal Health Coverage (UHC)) hapa nchini.
Ameongeza kuwa wakati viwango vya vifo vya kina mama Tanzania vimepungua kwa kiasi kikubwa, kutoka 760 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2000 hadi 238 mwaka 2020, pia vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano vimepungua.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ismail Rumatila, ameishukuru Japan kwa msaada huo akisema utasaidia kununua vifaa katika hospitali saba za rufaa vitakavyoongeza uwezo mkubwa wa uchunguzi na matibabu.



