CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeishukuru serikali kwa kukipatia fedha zaidi ya Sh bilioni 70 ambazo zinazotarajia kuboresha miundombinu ya majengo na ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa vya kufundishia kwa lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo katika mkutano wa pili wa mwaka wa Majilisi wa SUA ambao unahusisha watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya serikali na yasiyo ya Serikali.
Profesa Chibunda amesema wanafunzi zaidi ya 22 ,000 kutoka ndani na nje ya nchi wameomba kujiunga na masomo katika chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2024 huku nafasi zikiwa 7,000 pekee .
Amesema idadi hiyo inaakisi ubora wa chuo hicho unaondelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Profesa Chibunda amesema kwa kutambua umuhimu na ubora wa chuo hicho, serikali ya awamu ya Sita imekipatia Sh bilioni 70 katika kipindi cha miaka minne kwa ajili ya kuboresha miundombinu.
“Tayari kuna ujenzi utaanza kuanzia mwezi ujao na tupo katika hatua ya mwisho ya kupata wakandarasi na baada ya hayo majengo chuo chetu sura yake itabadirika zaidi na idadi ya wanafunzi itazidi kuongezeka,” amesema Profesa Chibunda.
Profesa Chibunda amesema katika kuhakikisha SUA inaendelea kutoa wahitimu wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri imeendelea kuboresha miundombinu ya kufundisha ikiwa ni pamoja na kufanya mafunzo kwa vitendo ambapo hivi sasa kimenunua gari ya kuchimba visima kwa zaidi ya sh milioni 200 na kuishukuru Serikali kwa kuwezesha mpango huo.
“SUA ni Chuo pekee kinachofundisha Uhandisi wa Umwagiliaji hivyo ingekuwa ajabu mhandisi anatoka SUA hata gari tu la kuchimba visima hajui linafanyaje kazi…,SUA siyo mahali pa kuigiza kama mwanafunzi amekuja kusoma mfano matibabu ya Wanyama kama ni ng’ombe basi ataangushwa kweli na kutibiwa ili apone” amesema Profesa Chibunda.
Profesa Chibunda amesema SUA itaendelea kuboresha na kuimarisha idara zilizopo ili ziwe na vitendea kazi vya kisasa zaaidi ambavyo vitawawezesha wanafunzi wanaohitimu wasiwe ni wa kwenda kutembea na bahasha kutafuta kazi bali wawe wamewiva na kutofikiria kuajiriwa .
Mkurugenzi wa Kampuni ya Afya ya Mnyama Digital ambaye ni mmoja wa wahitimu ya chuo hicho, Marko Mabula ametumia mkutano huo wa pamoja kuvishauri vikuu nchini kuwekeza kwa vijana wanaochipukia kwa kuwapa usaidizi wa namna ya kuwapa mitaji wakiwa bado ni wanafunzi .
Mabula amesema usaidizi huo utawawezesha kuendeleza mawazo waliyonayo kama ambavyo SUA inavyotoa usaidia huo kwa wanafunzi wake kwa kuwapa njia ya namna ya kupata mitaji ambayo inawawezesha kutengeneza ubunifu na kuuendeleza.
“Kuna haya ya Vyuo Vikuu nchini kutengeneza mazingira ya vijana wao ili waweze kujiajiri mapema na kupugunza wimbi la ukosekanifu wa ajira punde wanapomaliza masomo yao” amesema Mabula.
Mabula amesema usaidizi huo utawawesha wahitimu wa vyuo vikuu kujiajiri wao na pia kutengeneza ajira kwa vijana wenzao na hivyo kupunguza utegemezi kwa serikali pamoja na wimbi la vijana wanaokosa kazi.