Bil 82/- kutekeleza miradi Muleba 2025/2026

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wamepitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka  wa fedha 2025/2026 kiasi cha Sh bilioni 82.27 huku wakijipanga kukusanya mapato ya ndani kutoka Sh blioni 8.8 hadi bilioni 9.2

Akiwasilisha taaarifa ya Rasimu Mpango wa Bajeti mbele ya baraza hilo, Ofisa Mipango wa Halmashauri,  Evarth Kagaruki amesema bajeti hiyo imezingatia vipaumbele mbalimbali vya halmashauri na namna bora ya kubuni vyanzo vipya vya kukusanya mapato ili kukidhi mahitaji mbalimbali  ya wananchi wa Wilaya ya Muleba.

Advertisement

Alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni  ukamilishaji wa miradi yote viporo, kuimarisha miundombinu katika maeneo ya kutolea huduma, kutekeleza miradi ya kimkakati kwa lengo la kuongeza bajeti ya ndani , uboreshaji wa huduma za elimu na afya, kuendesha vikao kisheria, kulipa mishahara ya watumishi, kuendelea kutoa elimu ya uraia kwa wananchi pamoja na utunzaji wa mazingira.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Justus Magongo amesema kumekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mapato katika sekta ya uvuvi ambayo inachangia mapato kwa asilimia 43 katika halmashauri hiyo kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo halmashauri hiyo inalenga kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kukamilisha malengo ya wananchi na mahitaji  ya halmashauri hiyo.

“Kwa asilimia kubwa wilaya hii imezungukwa na visiwa ndani ya Ziwa Victoria hivyo mapato makubwa yanatokana na uvuvi ,ingawa kwa kipindi cha hivi karubuni kuna mabadiliko makubwa ya tabia ya nchi hivyo najua wasiwasi uliopo juu ya mchango wa sekta hii, tayari tumekaa na wataalam na tumepata vyanzo vipya ili Kuhakikisha bajeti yetu haitikisiki,”amesema Magongo.

Baadhi ya Madiwani wa Baraza hilo wamepongeza  ongezeko la bajeti hiyo  ambayo imetoka Sh bilioni  76.99  mwaka 2024/2025 hadi Sh bilioni 82.27  mwaka wa fedha 2025/2026 na kudai kuwa hakuna  sekta ya wananchi ambayo haikuguswa hivyo wananchi wa wilaya hiyo watarajie maisha bora na huduma bora.

“Wananchi wetu tunaowaongoza wanachokitaka ni maisha yenye unafuu, huduma bora za kisasa  ,mazingira safi ya uzalishaji na masoko ya kuuza bidhaa kwa bajeti ambayo tumepitisha yote yamezingatiwa na tunaamini Baraza la Madiwani na wataalamu wa halmashauri wote tutaungana kufanya utekelezaji kwa lengo moja kurahisisha maisha ya wananchi wetu wanaoishi vijijini,”amesema Theobard Michael Diwani wa Kata Kasharunga.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *