Biteko ataka bajeti ajenda ya wanawake, amani, usalama

SERIKALI imeagiza wizara, taasisi za serikali na wadau wa maendeleo watenge bajeti ya kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alitoa agizo hilo wakati anazindua mpangokazi wa kitaifa wa kutekeleza mpango huo katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (TPTC) Kunduchi mkoani Dar es Salaam.

“Wizara zote zenye dhamana ya agenda hii, Tanzania Bara na Zanzibar mkasimamie na kutekeleza mpango huu kama ilivyokusudiwa ili kufikia malengo stahiki,” alisema Dk Biteko.

Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie utekelezaji wa mpango huo kwa kushirikiana na wadau waliopo.

“Niwaombe kuhakikisha kuwa mnatoa elimu na kuhamasisha, ushiriki wa wanawake na wanaume katika hatua zote za kuzuia, kutatua migogoro na ujenzi wa amani, ulinzi na usalama,” alisema Dk Biteko.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema katika kuandaa mpango huo, uainishaji wa maeneo mahususi ya vipaumbele vya mpango umezingatia maudhui ya Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Dk Gwajima alisema mpango huo unabainisha maeneo manne ya kipaumbele likiwemo la kuzuia linalosisitiza umuhimu wa kujumuisha mitazamo ya kijinsia katika mikakati ya kuzuia migogoro na mbinu za tahadhari za mapema.

Lingine ni la ushiriki linalosisitiza haja ya ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi katika ngazi zote katika michakato ya amani, utatuzi wa migogoro na kujenga amani.

Alitaja maeneo mengine kuwa ni ulinzi linalotoa mwito wa kuimarishwa kwa hatua za kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia wakati na baada ya migogoro na eneo la msaada na urejeshaji wa hali.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alisema Tanzania imetambua kuwa ili kuimarisha amani wanawake lazima washirikishwe katika ajenda hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Zanzibar (SMZ), Riziki Pembe alisema Ajenda ya Wanawake Amani na Usalama ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na Watanzania wote.

Riziki alisema SMZ imeweka mikakati na mipango kuhakikisha wanawake wanashirikishwa katika masuala ya amani na usalama na kukuza usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button