Biya ajiimarisha kijeshi kabla ya uchaguzi

YAOUNDE : RAIS wa Cameroon, Paul Biya (92), ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani, amefanya mabadiliko makubwa katika safu ya juu ya jeshi la nchi hiyo, hatua ambayo wachambuzi wanaitafsiri kama jitihada za kuimarisha ushawishi wake kuelekea azma ya kugombea muhula wa tisa.
Katika mabadiliko hayo, Biya amewateua makamanda wapya wa jeshi la ardhini, jeshi la anga na wanamaji. Aidha, amewapandisha vyeo mabrigedia wanane kuwa majemedari wa ngazi ya meja jenerali.
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo ni mratibu wa kikosi maalum cha Rapid Intervention Battalion (BIR), ambacho ni sehemu muhimu ya vyombo vya usalama na kinahusika na operesheni dhidi ya ugaidi nchini humo.
Pamoja na hayo, Rais Biya amemteua mshauri mpya maalum wa rais kuhusu masuala ya kijeshi, hatua inayoashiria kuimarika kwa udhibiti wa safu ya kijeshi katika kipindi hiki cha maandalizi ya kisiasa.



