Bodi EWURA yakagua Bomba la Mafuta TAZAMA

DAR E SALAAM: MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Prof Mark Mwandosya ameongoza wajumbe wa bodi hiyo na menejimenti kukagua Bomba la Mafuta la TAZAMA linaloanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia kwa lengo la kufahamu changamoto za kiuendeshaji na kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyoanza Machi 21, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ya Bodi ya EWURA, Ngosi Mwihava alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua uendeshaji wa bomba la TAZAMA na masuala yote ya kiuchumi na kimiundombinu.
“Moja ya jukumu la EWURA katika sekta ya petroli ni kudhibiti miundombinu inayohusu ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia, hivyo ziara hii ni mahususi kwa ajili ya kukagua bomba, kuona changamoto zilizopo na kuangalia namna tunavyoweza kusaidia utatuzi wa changamoto hizo ili kuendelea kuboresha huduma za usafirishaji wa mafuta kupitia bomba hili,” Mwihava alisema.
Mwihava aliongeza pia kuwa ziara hiyo ni fursa ya Bodi ya EWURA na ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya upangaji wa bei, mikakati ya uhifadhi wa mafuta ya akiba na kujengea wataalamu uwezo
Ujumbe huo umetembelea kituo cha Chilolwa cha kuangalia usalama wa bomba la mafuta, kituo cha kusukuma mafuta kilichopo Chinsali na ghala la kuhifadhia mafuta lililopo Mpika.
SOMA: Ewura yamwaga mamilioni Iringa
Maeneo mengine yaliyotembelewa ni kituo cha Kilonje cha kusukuma mafuta, kituo cha Mulilima cha kutuma na kupokelea kifaa cha kufanya usafi wa bomba, na kituo cha kupokelea mafuta cha Bwana Mkubwa terminal ambacho kiko Ndola.
Ujumbe huo pia ulitarajiwa kukutana na uongozi la Bomba la TAZAMA, Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) pamoja na Baraza la Mazingira Zambia (NWASCO) ili kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kisekta.
Tazama ilianzishwa mwaka 1968 kwa lengo la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania hadi Zambia japokuwa teknolojia hiyo ilikuja kubadilishwa baadaye na kusafirisha bidhaa hiyo iliyokamilika katika mnyororo wake wa uzalishaji.
Bomba hilo linasafirrisha mafuta kwa umbali wa kilomita 1,710 unaohusisha urefu wa kilomita 954 kwa bomba lenye kipenyo cha inchi nane na kilomita 798 kwa bomba lenye kipenyo cha inchi 12.
Inakadiriwa , bomba hili husafirisha takribani mafuta yenye ujazo wa tani 800,000 kwa mwaka.