MWANZA: BODI ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesema inategemea mafanikio makubwa katika kuiwezesha wakala hiyo kutimiza azma yake ya kuwafikishia wananchi walioko vijijini nishati bora za umeme, mafuta na gesi.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kikao cha kwanza cha bodi hiyo mpya kilicholenga kutambuana na kupanga majukumu.
“Kikao chetu kimeenda vizuri, tumechagua kamati na kupangiana majukumu tunaamini na tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu sawasawa na sheria iliyoanzisha Wakala wa Nishati Vijijini inavyoelekeza,”… Alisema
Aidha katika hatua nyingine Balozi Kingu amemshukuru, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi na amemshukuru Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwa kukamilisha mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa bodi, jambo ambalo limeiwezesha kuwa bodi kamili.
Akieleza zaidi kuhusu majukumu waliyojipangia, Balozi Kingu amesema mapema Mwezi Machi, bodi itakutana katika kikao cha dharura kupitia na kujadili masuala mbalimbali ya Wakala ambayo yalikuwa yakisuburi baraka za bodi ili kuyatolea maamuzi yatakayowezesha utekelezaji wake kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu wa bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amepongeza Mamlaka za Uteuzi, kuteua watu makini, hodari na wachapakazi ambao amesema ni muhimu kuwa nao katika kuisimamia Wakala hiyo yenye majukumu makubwa yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, ametoa ahadi ya ushirikiano kwa bodi hiyo mpya ili kuhakikisha malengo ya Serikali kupitia majukumu yaliyokasimiwa kwa wakala yanatekelezwa.
Ikumbukwe Januari 26 mwaka huu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliwateua Florian Otman Haule, Lucas Charles Malunde, Mwantum Issa Sultan, Stephen Menard Mwakifamba, James Issack Mabula, Ahmed Martin Chinemba, Sophia Shaban Mgonja na Balozi Radhiya Naima Msuya kuwa Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, wakiungana na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Septemba 2023 kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo.