Bodi ya Ithibati ya Wanahabari kuzinduliwa Machi 3

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi wiki ijayo anatarajiwa kuzindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa imeeleza uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Machi 3, Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, Kabudi pia atamkabidhi zana za Kazi Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando zinazojumuisha Sera ya Habari, Sheria ya Huduma za Habari na kanuni zake.
Miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo yanayotarajiwa kuanza kutekelezwa mapema baada ya kuzinduliwa ni pamoja na kutoa Ithibati na Vitambulisho kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo vilivyoainishwa kisheria na kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imepewa mamlaka ya kutoa vitambulisho kwa waandishi wote kutoka vyombo vya habari vya umma, binafsi na waandishi wa kujitegemea.
Awali, utoaji wa vitambulisho hivyo kwa waandishi wa habari ulikuwa ukifanywa na Idara ya Habari-MAELEZO kabla Bodi ya Ithibati kuundwa na kuanza majukumu yake rasmi.
Baadhi ya majukumu mengine ya bodi hiyo ni kuishauri serikali kuhusu mafunzo ya uandishi wa habari na mitaala inayofundishwa vyuoni, kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu maadili ya uandishi wa habari, kushirikiana na taasisi nyingine hususani vyuo vikuu kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari.
Bodi hiyo ilitangazwa Septemba 18, mwaka jana baada ya Waziri mwenye dhamana kumteua, Mhando na wajumbe wengine sita kuunda bodi hiyo, sanjari na kuwahamishia watumishi sita kutoka wizarani kuunda Sekretarieti ya bodi hiyo.
Wajumbe wa bodi hiyo pamoja na Tido ni Thobias Makoba, Mgaya Kingoba, Dk Rose Reuben, Dk Egbert Mkoko na Ladislaus Komanya.



