BENKI Kuu ya Tanzania na Bodi ya Bima ya Amana (DIB) inashiriki maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba.
Maonesho hayo yamezinduliwa Oktoba 10, 2024 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Maonesho hayo yameanza Oktoba 7, na yanatarijwa kumalizika Oktoba 20, 2024 yakiwa na kauli mbiu “Haki ya Chakula kwa Maisha Bora ya sasa na baadaye”.
SOMA: Makamu wa Pili wa Rais SMZ ahimiza mazoezi
Mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kupitia maadhimisho hayo watu watajifunza kuhusu vyakula vya asili vinavyopatikana kwenye visiwa vya Pemba na Unguja sambamba na kutoa elimu ya lishe, ili kupunguza tatizo la udumavu kwenye jamii.
Wakati huo huo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamata Shaame Khamis ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Bodi ya Bima ya Amana kwa kushiriki maonesho hayo yanayofanyika viwanja vya Chamanangwe Kisiwani Pemba.