BoT, Mtwara wajadili uchumi, uwekezaji

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, pamoja na viongozi wengine wa mkoa kujadili maendeleo ya kiuchumi na fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo.

Katika kikao hicho Gavana Tutuba amesema kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kufanya vizuri kutokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha.

Amebainisha kuwa Benki Kuu itaendelea kuisimamia kikamilifu sekta ya fedha ili iwe chachu ya ukuaji wa uchumi na kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050, inayolenga kufikia uchumi wa Dola trilioni 1 kutoka Dola bilioni 85 za sasa.

SOMA: Benki Kuu yatoa elimu mikopo salama

Aidha, Gavana amehimiza wananchi kushiriki zaidi katika sekta za uzalishaji kama kilimo, uvuvi, ufugaji wa mifugo na nyuki, huku akiwahamasisha wakulima kutumia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ili kunufaika zaidi na mazao yao.

Pia Gavana Tutuba amesisitiza umuhimu wa miradi ya maendeleo kutekelezwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Amebainisha kuwa majadiliano ya mradi mkubwa wa gesi asilia (LNG) yanatarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao, mradi ambao utachochea ukuaji wa uchumi wa Mtwara na taifa kwa ujumla.

Katika ajenda ya elimu ya fedha, Gavana Tutuba alisema kuwa BoT tayari imeandaa mitaala na ipo tayari kushirikiana na mkoa wa Mtwara ili kuimarisha uelewa wa wananchi na watumishi wa umma katika masuala ya kifedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amempongeza Gavana Tutuba kwa mchango mkubwa wa Benki Kuu katika kuimarisha uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 85 ya uchumi wa mkoa huo unatokana na kilimo cha korosho, mbaazi, ufuta, choroko na mazao mengine.

Mkuu wa Mkoa pia ameeleza hatua kubwa zilizopatikana katika sekta za miundombinu, ikiwemo upanuzi wa bandari yenye uwezo wa kuhudumia tani milioni 2 kwa mwaka, uboreshaji wa uwanja wa ndege kwa kuweka taa za usiku, pamoja na ujenzi wa barabara zinazounganisha wilaya za mkoa huo.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na uongozi wa Tawi la Benki Kuu la Mtwara likiongozwa na Mkurugenzi wa Tawi, Nassor Nassor.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button