Benki Kuu yatoa elimu mikopo salama
Ni baada ya wananchi wa Iringa kulalamika mikopo umiza

IRINGA: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeingia kwa kishindo mkoani Iringa kutoa elimu kwa umma kuhusu mikopo salama, baada ya ripoti ya uchunguzi kubaini kuwepo kwa ongezeko la mikopo kandamizi isiyo rasmi maarufu kama “mikopo umiza” au “kimangala”.
Mikopo hiyo imeelezwa kudumaza maendeleo ya kiuchumi ya wakazi wa mkoa huo.
Ripoti hiyo iliyofanyika kati ya Aprili na Mei mwaka huu, ilionesha kuwa wakazi wa Iringa wengi wamekuwa wakikopa kutoka kwa watu au taasisi zisizosajiliwa, hali inayowaweka hatarini kupoteza mali zao, kubughudhiwa, au kuingia kwenye madeni yasiyoisha kutokana na masharti magumu ya mikopo hiyo.
Akizungumza wakati BOT ikitoa elimu kwa wadau wa masuala ya fedha wa mjini Iringa, Afisa Sheria Mwandamizi wa BoT na mtatuzi wa malalamiko ya wateja wa huduma za kibenki, Ramadhani Myonga, alisema elimu wanayoitoa inalenga kuwawezesha wananchi kutambua taasisi halali za kifedha zilizosajiliwa na benki hiyo na kuepuka mitego ya wakopeshaji wasio rasmi.
“Watu wengi wanakopa bila kuelewa hatari zilizopo. Wengine hawajui kuwa wanaruhusiwa kuomba leseni ya utoaji huduma za kifedha. Hii elimu inasaidia pia kwa wakopeshaji kuhalalisha shughuli zao,” alisema Myonga.
Alisema, ikiwa elimu hiyo itafika kwa walengwa, italeta utulivu wa kifedha kwa mtu mmoja mmoja na kuchangamsha uchumi wa eneo hilo.
Alieleza kuwa mikopo salama huambatana na mkataba rasmi unaoeleweka na mteja, na taasisi husika lazima iwe na leseni kutoka BoT.
Myonga aliwaasa wananchi kuhakikisha kuwa kabla ya kukopa, wanazisoma kwa umakini nyaraka za mkataba wa mkopo, kuelewa vipengele vyake, na kuhoji masuala yanayowatatiza kabla ya kusaini.
Aliongeza kuwa kila taasisi ya fedha lazima iwe na dawati la kushughulikia migogoro baina yao na wateja, ambapo mgogoro unatakiwa kutatuliwa ndani ya siku 14, na ikiwezekana kuongezewa siku saba kabla ya kufikishwa BoT kwa hatua zaidi.
“Mkopo si sadaka. Rejesha kwa wakati, tunza kumbukumbu zako, hifadhi nyaraka za mkopo wako, na usikurupuke kukopa kwa ajili ya sherehe au matumizi yasiyo ya msingi,” alisisitiza.
Afisa huyo pia alibainisha kuwa ni haki ya mkopaji kupewa elimu kuhusu mkopo anaotaka kuchukua, lakini pia ni wajibu wake kurejesha mkopo kwa wakati na kuhakikisha taasisi anayokopa ina leseni halali.
Alisema kuwa BoT inaendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo nchi nzima kwa lengo la kujenga jamii yenye maarifa ya kifedha.
Kwa upande wake, Mchungaji Ombeni Sawike, mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, alieleza jinsi elimu hiyo ilivyomfungua macho kuhusu uwekezaji katika mifuko rasmi ya fedha na umuhimu wa kuelimisha jamii.
“Nilikuwa sijui kabisa kuhusu leseni za taasisi za kifedha wala haki za mkopaji. Sasa naweza kuwaelimisha watu wengine kuhusu madhara ya mikopo umiza na jinsi ya kuchagua taasisi sahihi za kukopa,” alisema Sawike.
Aliwasihi wananchi kuwa makini kabla ya kuchukua mikopo, wakihakikisha kuwa wanakopa kwa malengo yenye tija na kutoka kwa taasisi zinazoendeshwa kwa mujibu wa sheria.
Alishukuru kampeni hiyo ya BoT akisema ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kifedha na kuepuka kuingia kwenye madeni yanayowapokonya mali au kuwasababishia machungu makubwa ya kifamilia na kijamii.