BoT yatoa hakikisho usalama mifumo ya malipo

DODOMA: Benki Kuu ya Tanzania imekanusha taarifa kuhusu usalama mdogo wa mifumo ya malipo na akaunti za amana katika benki na taasisi za fedha.

Taarifa iliyotolewa na benki hiyo jana na kusainiwa na Gavana, Emmanuel Tutuba imeeleza kuwa taarifa hizo potofu zinalengo la wateja kuondoa fedha zao kwa hofu kuwa mifumo hiyo itashambuliwa na wahalifu wa kimtandao.

“Benki Kuu inawahakikishia wananchi kuwa mifumo ya malipo ya taifa pamoja na amana za wateja katika benki za biashara ni salama na inaendelea kuzisimamia kwa ufanisi na tija inayostahiki,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia Benki Kuu imewaonya wanaosambaza taarifa hizo kuacha haraka kwani vitendo hivyo havina tija katika maendeleo ya sekta ya fedha au uchumi wa mmoja mmoja na taifa.

Aidha, kwa watakaopatikana kuhusika na vitendo hivyo, benki hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, benki hiyo imewashauri wananchi kuendelea kutunza amana zai katika benki kwani kuna manufaa mengi, ikiwemo pesa kuongezeka kutokana na malipo ya riba au faida ya mwaka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button