Boti za bil 1/- kuimarisha uvuvi mwambao Ziwa Tanganyika

KIGOMA: SERIKALI imekabidhi boti 19 zenye thamani ya Sh bilioni 1.1 za uvuvi na doria kwa ajili ya kuimarisha uvuvi kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede alikabidhi boti hizo katika Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha shughuli za uvuvi zinakuwa na tija.

Katika boti zilizokabidhiwa zipo boti 11 kwa ajili ya kufanya doria kwenye mwambao Ziwa Tanganyika zenye thamani ya Sh milioni 539 ambazo zimekabidhiwa kwa vikundi vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi Ziwa Tanganyika (MBU’s) sambamba na boti nane za kisasa za uvuvi zenye thamani ya Sh milioni 607.3 .

SOMA ZAIDI: Serikali yaeleza mafanikio mifugo, uvuvi

Naibu Katibu Mkuu huyo pamoja na boti amekabidhi pia vifaa vya kuvulia ikiwemo kifaa cha kuangalia wingi wa samaki (Fish Finder), nyavu, maboya na vifaa muhimu za kusaidia uvuvi wa kisasa wenye tija.

Akizungumza kabla ya kukabidhi boti hizo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede amesema serikali imedhamiria kuona shughuli za uvuvi zinafanyika kisasa ili kuwezesha kupata uzalishaji mkubwa wa mazao ya uvuvi na kuimarisha uchumi wa wavuvi na kuongeza mapato ya serikali.

Awali, Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara hiyo, Profesa Mohamed Sheikh alisema  kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Rais Samia ametoa Sh Bilioni 11.5 kwa ajili ya ununuzi wa boti za kisasa 120 za uvuvi na doria nchini na vifaa vya kisasa vya uvuvi ambapo kati ya hizo Ziwa Tanganyika limepatiwa boti 19 ambazo tayari zimetolewa.

Profesa Sheikh alisema kuwa boti hizo zitawezesha wavuvi kwenda kwenye maji ya kina kirefu kwa ajili ya kuvua hivyo kuondokana na tabia ya kuvua pembezoni mwa ziwa ambako kuna mazalia ya samaki sambamba na boti za doria ili kuzuia uvuvi kwenye maeneo tengefu kwa ajili ya mazalia ya samaki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button