SERIKALI imeeleza mafanikio katika sekta za mifugo na uvuvi.
Imesema mauzo ya nyama nje yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2021 hadi kufika tani 14,701 na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Pia, mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka tani 167.3 mwaka 2020 hadi kufika tani 181.6 kwa sasa.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo Rufiji mkoani Pwani jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).
Msigwa alisema serikali imeendelea kuwawezesha wananchi kwa kuwapa dawa za mifugo na elimu ya ufugaji wa kisasa na matokeo yameanza kuonekana.
Katika hilo alisema mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2021 hadi kufika tani 14,701 kwa sasa, hatua inayochangia fedha za kigeni nchini zilizopatikana kuwa Dola za Marekani milioni 61.39.
Aidha, katika hilo idadi ya viwanda vilivyothibitishwa kuuza nyama nje ya nchi vimeongezeka kutoka vinne hadi kufika sasa, na kuwa Diplomasia ya uchumi imefungua masoko ya nyama nchini na sasa inauzwa katika mataifa 12 ya nje.
Alitaja baadhi ya mataifa hayo ni Comoro, Falme za Kiarabu (UAE), Kuwait, Hong Kong, Jordan, Saudia, Vietnam, Qatar, Rwanda, Kenya na Oman.
Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi imetenga hekta 11,754 za malisho, kwa kuwa kuna changamoto ya maeneo ya malisho na kuwa vijiji 48 vimetengewa maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji ili waweze kufuga na kupata malisho.
Katika hilo alisema serikali pia imesambaza tani 33,359 mbegu za malisho katika maeneo mbalimbali ili wafugaji wapate malisho na kuzalisha mifugo yenye vigezo vya ubora wa nyama inayokubalika katika masoko ya ndani ya kimataifa.
Uvuvi
Msigwa alisema serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ili nchi inufaike na uvuvi mkubwa.
Alisema katika mradi huo ujenzi wake umefikia asilimia 79 na kunajengwa gati kwa ajili ya kupokea meli za uvuvi ambao ujenzi wake umefika asilimia 98. Lakini pia kunajengwa jengo la utawala ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 90 na jengo la kuhifadhi samaki ambalo limefikia asilimia 65.
“Tukikamilisha ujenzi wa bandari hapa tutawezesha meli zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki hivyo kuchochea uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi,” alisema Msigwa.
Alisema uwekezaji huo unakwenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.5 hadi 52,937.99 na kwamba ikifikia hapo serikali itakuwa imeongeza mchango wa fedha za kigeni kwenye pato la taifa.
Msigwa alisema katika hilo serikali iliweka mkakati wa kuongeza tija kwenye sekta ya uvuvi kwa kununua boti za uvuvi 160 ambazo zilisambazwa kwa wananchi 3,163 kati yao wanawake ni 1,008 wanaume 2,115 ili wavue kisasa.
Aidha, serikali ilitekeleza mradi wa vizimba katika Ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo mengine ya Bahari ya Hindi ambapo jumla ya vizimba 274 vilijengwa kwa kuwakopesha wananchi fedha.
Katika hilo alisema wananchi 1,250 walinufaika na Sh bilioni 5.6 zilizotumika kujenga vizimba hivyo na matokeo chanya yameanza kuonekana.
“Tunawawezesha wavuvi, tunataka wanufaike na fursa za uvuvi, tayari vikundi vinane vimeanza kupata faida, wamevuna samaki tani 83.2 na wamepata Sh milioni 645, si haba tumeanza, hatukuzoea utamaduni wa kufuga samaki huko nyuma,” alisema Msigwa.
Alisema kwa ujumla serikali imefanikiwa kuongeza tija kwani mazao ya uvuvi yameongezeka kutoka tani 167,256 ambazo zina thamani ya Dola za Marekani milioni 813 mwaka 2020 hadi kufika tani 181,655.70 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 878.88.