Mafunzo kuongeza ufanisi kwa wajasiriamali

IRINGA: ZAIDI ya wajasiriamali 300 kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Iringa Mjini wamehitimu mafunzo maalumu ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Fadhili Ngajilo.

Mafunzo hayo yana lengo la kuwaongezea uwezo wa kushindana katika soko, kuboresha biashara zao na kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo, yaliyowakutanisha wafanyabiashara wadogo, vijana na wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, yalilenga kuwajengea uwezo katika maeneo ya usimamizi wa biashara, upatikanaji wa mitaji, masoko, matumizi ya teknolojia pamoja na mbinu za kisasa za uendeshaji wa biashara.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, mgeni rasmi Christina Makweyi aliwataka washiriki kutumia maarifa waliyojifunza kama nyenzo ya kubadilisha maisha yao na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa.

Alisema mafunzo hayo yanakuja wakati muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kukuza uchumi wa wananchi kupitia sekta binafsi na shughuli za ujasiriamali.

“Maarifa mliyopata hapa yawe mwanzo wa safari mpya ya mafanikio. Ujasiriamali wa sasa unahitaji ubunifu, nidhamu ya fedha na uwezo wa kuziona na kuzitumia fursa zilizopo katika soko,” alisema Makweyi.

Aliwahimiza wajasiriamali hao kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuongeza mitaji na kupanua biashara zao.

Pia aliwataka kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na ushirika, akieleza kuwa vikundi hivyo vinarahisisha upatikanaji wa mikopo, mafunzo na masoko, huku vikiongeza nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto za biashara.

Makweyi alisisitiza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii, kama nyenzo muhimu ya kutangaza bidhaa na huduma, kuwafikia wateja wengi zaidi na kuongeza ushindani katika soko la kisasa.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa wamepata maarifa mapya yatakayowasaidia kuboresha usimamizi wa biashara zao, kuongeza faida na kuendesha shughuli zao kwa weledi zaidi.

Walimpongeza Mbunge huyo, kwa kuandaa mafunzo hayo wakisema ni hatua muhimu ya kuwainua kiuchumi wananchi wa jimbo hilo, hususan vijana na wanawake ambao ndiyo nguvu kazi kubwa ya taifa.

Washiriki hao walibainisha kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya wa namna ya kuandaa mipango ya biashara, kutunza kumbukumbu za kifedha, kutafuta masoko na kutumia fursa mbalimbali za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali na taasisi binafsi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mbunge huyo za kuendelea kuwajengea uwezo wananchi wake ili waweze kujitegemea kiuchumi, kuongeza ajira na kuchangia maendeleo ya mkoa wa Iringa na nchi kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button