Kilimo kuongoza ajenda mabadiliko ya uchumi

DODOMA:Serikali imesema itatoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27, ikiitaja kuwa miongoni mwa sekta zitakazochochea mageuzi ya uchumi, kuongeza uzalishaji na kufungua fursa za ajira nchini.
Akiwasilisha mpango huo bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kilimo, mifugo, uvuvi na misitu zimeainishwa kama sekta muhimu katika juhudi za kuimarisha uchumi na kuhakikisha usalama wa chakula.
Mkumbo amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta hizo ili kuongeza tija, kuimarisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani na kuongeza kipato cha wananchi, hususan wanaotegemea shughuli za kilimo.
“Kilimo kinaendelea kuwa mwajiri mkubwa zaidi nchini na nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wetu,” alisema Profesa Mkumbo.
Hata hivyo, alionya kuwa changamoto za mazingira ya kimataifa zinaweza kuathiri upatikanaji na gharama za baadhi ya pembejeo muhimu za kilimo, hususan mbolea.
“Tanzania huagiza asilimia 30 hadi 40 ya mbolea aina ya Urea na DAP kutoka nchi za Ghuba,” alisema, akieleza kuwa migogoro inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati inaweza kuongeza gharama za bidhaa hizo na kuathiri shughuli za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Serikali, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, ikiwemo kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa pembejeo na bidhaa nyingine muhimu kwa uchumi.
Mkazo huo unalenga kuongeza ustahimilivu wa sekta ya kilimo dhidi ya misukosuko ya soko la kimataifa na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.



