Bolsonaro ahukumiwa miaka 27 jela

BRAZIL: RAIS wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro, amehukumiwa kifungo cha miaka 27 na miezi mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kupanga njama za kufanya mapinduzi ya serikali.
Hukumu hiyo imetolewa na majaji wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo baada ya kumtia hatiani kwa makosa matano, ikiwemo kosa la kujaribu kumuua Rais wa sasa, Luiz Inácio Lula da Silva, na jaribio la kubatilisha utaratibu wa kidemokrasia. SOMA: Majaji wamtia hatiani Bolsonaro
Majaji wanne kati ya watano wa jopo hilo walikubaliana Alhamisi, Septemba 11, kwamba Bolsonaro alihusika moja kwa moja katika mipango ya kubaki madarakani licha ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Mbali na Bolsonaro, watuhumiwa wengine kadhaa pia walihukumiwa, akiwemo Waziri wa zamani wa Ulinzi, Jenerali Braga Netto, ambaye alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 26 jela. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, makosa yaliyomhusisha Bolsonaro ni pamoja na kuongoza genge la kihalifu, kuandaa njama ya mapinduzi ya kijeshi, na kuharibu mali za umma.
Hata hivyo, mawakili wake wamepinga hukumu hiyo na tayari wametangaza mpango wa kukata rufaa wakisisitiza kuwa mteja wao hana hatia. Awali, Bolsonaro alikuwa chini ya kifungo cha nyumbani mjini Brasília wakati kesi ikiendelea kusikilizwa.



