Muziki ni biashara, usajili ni kinga

DAR-ES-SALAAM : WASANII wa muziki nchini wametakiwa kusajili na kulinda kazi zao kupitia mifumo rasmi ya miliki bunifu ili kunufaika kiuchumi na kuzuia wizi wa kazi zao za ubunifu.
Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu Duniani kwa mwaka 2025 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Nyaisa amesema kuwa licha ya mafanikio ya muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya kimataifa, wasanii wengi bado hawajasajili rasmi kazi zao, jambo linalowanyima haki na mapato stahiki kwa mujibu wa sheria.
SOMA : Wasanii wapewa somo kuelimisha jamii
“Tunasisitiza kuwa muziki si burudani tu, ni biashara. Na kila biashara inahitaji kulindwa. Wasanii wengi wanapoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” amesema. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Muziki na Miliki Bunifu Tanzania: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.”
Ameongeza kuwa BRELA inaendelea kutoa elimu kwa wasanii kuhusu haki zao za ubunifu na kuwawezesha kufikia huduma muhimu za usajili ili wajue namna bora ya kulinda kazi zao.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alipongeza kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu, akieleza kuwa ni dira muhimu ya kuendeleza na kulinda ubunifu nchini.