Bunge kumpongeza Rais Dk Samia leo

DODOMA; Mkutano wa Tano wa Bunge la 13 unaanza leo jijini Dodoma  ukitarajiwa pamoja na shughuli nyingine kuwa na maazimio matatu likiwamo la kumpongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuwezesha kufanyika nchini Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Aidha, mkutano huo utajadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2027/2028.

“Katika Mkutano wa Tano wa Bunge, jumla ya maazimio matatu yatawasilishwa na kujadiliwa na bunge kwa ajili ya kupitishwa,” ilisema taarifa iliyotolewa jana na ofisi bunge.

Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU ulifanyika kuanzia  Oktoba 5 hadi 9 mwaka huu jijini Arusha.

Kulingana na ratiba iliyotolewa, azimio la kumpongeza Rais Dk Samia kwa kuridhia mkutano huo ufanyike nchini litakuwa leo.

Azimio lingine ni la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Tanzania Kujiunga na Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Usalama wa Angamtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2014 (Mkataba wa Malabo). Lingine ni la Kuridhia Marekebisho ya Mkataba wa Kimataifa wa Sukari wa Mwaka 1992.

Wakati huo huo mkutano huo  wa bunge utakaoahirishwa Novemba 6 mwaka huu,  kutakuwa na kipindi cha maswali yatakayoulizwa na wabunge na kujibiwa na mawaziri.

Aidha, kutakuwa na kipindi cha maswali ya kwa papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu Alhamisi na takribani 16 yataulizwa na wabunge.

Vilevile kutakuwa na taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Pia kutakuwa na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button