Bunge laagiza NEMC kudhibiti muziki wa kelele kwenye makazi

BUNGE limeitaka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) idhibiti uchafuzi wa mazingira kupitia kelele zinazotokana na muziki au mambo mengine katika makazi ya watu.
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ametoa agizo hilo bungeni Dodoma jana wakati akiahirisha shughuli za Bunge. Zungu aliagiza NEMC itoe adhabu kali kwa wahusika kwa kuwa kelele zina athari kiafya kwa watu wakiwemo wazee.
Awali Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya (CCM) alisema baada ya saa nne usiku kelele na mitetemo kutoka katika vilabu na nyumba za ibada zimeendelea kuwaathiri watu kwa kuwakosesha usingizi.
Profesa Manya alisema inasikitisha muziki unapigwa kwa sauti ya juu na mitetemo hadi saa nane za usiku jambo ambalo halifai.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kelele na mitetemo katika makazi ya watu baada ya saa nne usiku siyo sawa, unalazimika kusikia muziki uliochaguliwa na kilabu hadi saa nane usiku, NEMC wanaweza kudhibiti,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Malleko alisema moto umekuwa ukiathiri Mlima Kilimanjaro kila mara na kusababisha vifo na serikali kutumia fedha nyingi kuukabili.