BUNGE limeazimia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha demokrasia na kukuza diplomasia ya uchumi.
Katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 11, Bunge pia limeazimia kumuunga mkono Rais Samia katika majukumu yake ya Rais wa Tanzania na kumwombea afya njema, baraka na ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa alisoma maazimio hayo bungeni jijini Dodoma jana na akasema katika miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia hali ya demokrasia na
utawala bora vimeendelea kuimarika nchini.
Chiwelesa alitaka mambo yaliyochangia kuimarisha demokrasia ni pamoja na uamuzi wa kuruhusu shughuli za siasa hasa mikutano ya hadhara kufanyika nchini kote.
“Uamuzi huu umefufua na kuimarisha shughuli za siasa nchini kwani vyama vya siasa vimepata fursa ya kunadi sera zao na kutoa mawazo mbadala ambayo yataisaidia
serikali kutekeleza huduma za kijamii na kiuchumi hususani masuala yanayogusa maendeleo ya wananchi,” alisema.
Alitaja jambo la pili ni kuanzisha vikao vya maridhiano ya kisiasa miongoni mwa
vyama vya siasa ili kuhakikisha kuna uhusiano mwema miongoni mwa makundi ya kisiasa yaliyokuwa yakihasimiana.
Chiwelesa alitaja jambo lingine ni kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya kimfumo na kisheria yanayoongoza shughuli za kisiasa; na kudumisha misingi ya amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Aliwaeleza wabunge kuwa pia demokrasia na utawala bora vimeimarika kwa kuridhia kuundwa kikosi kazi cha kufanyia kazi masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
“Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan ameonesha wazi nia yake ya kuifanya Tanzania kuwa moja, salama na bila kundi lolote kuwa nyuma katika kufurahia demokrasia ya kweli,” alisema Chiwelesa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imekuza diplomasia ya uchumi na yeye amekuwa chachu ya mafanikio hayo kwa kuwa mwanadiplomasia mahiri.
Alisema diplomasia ya uchumi imewezesha kuongezeka masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika masoko ya nje, kuimarika uhusiano wa kimkakati na kampuni za kimataifa unaolenga kuwekeza katika sekta za uzalishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Wabunge wameelezwa kuwa diplomasia hiyo pia imewezesha kupatikana misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka kwenye taasisi za fedha duniani inayosaidia kuboresha shughuli za maendeleo zikiwemo elimu, miundombinu, afya na maji.
Chiwelesa alisema diplomasia ya uchumi pia imekuza shughuli za uwekezaji na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji wapya kutoka nje ya nchi baada ya kufanyika maboresho ya mazingira ya kufanya biashara na pia filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” ametangaza vivutio vilivyopo nchini na hivyo kukuza sekta ya utalii.
Alisema diplomasia hiyo imeimarisha uhusiano na mataifa mengine na taasisi za kimataifa kutokana na ziara za Rais Samia nje ya nchi.