Burundi kuunganishwa na Mkongo wa Taifa

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesaini mkataba mpya wa kibiashara kwa ajili ya kuongeza huduma za mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na shirika la Burundi Backbone System (BBS) ya nchini Burundi.

Mkataba huo wa miaka mitano una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.3 Sawa na Sh bilioni 8.3 umesainiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na BBS.

Hafla ya kutia saini mkataba huo imefanyika  Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Peter Ulanga na Mtendaji Mkuu wa BBS,Jeremie Hageringwe huku ukishuhudiwa Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.

Akizungumza baada ya kutia saini Nape amesema uhusiano wa Tanzania na Burundi kupitia BBS ulianza mwaka 2019 wakati TTCL iliposaini mkataba wa kwanza wa kuwapa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Amesema mkataba huo ulihusisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa
Burundi-Burundi Backbone System kupitia eneo la Kabanga mpakani mwa Tanzania na
Burundi katika Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera na Manyovu upande wa Kigoma.

” Matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yamesababisha Serikali
ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo,” amesema na kuongeza kuwa mkataba mpya utaimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na utaboresha mawasiliano kati ya nchi hizi mbili.

Amesema Taifa linajivunia mchango mkubwa katika kuboresha mawasiliano katika Afrika Mashariki na kwamba mkataba mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania na Burundi kwa kuimarisha uchumi, biashara, na ushirikiano wa kijamii.

“Tunatoa shukrani zetu kwa Serikali ya Burundi na BBS kwa kuendelea kutuamini na
kutupa fursa ya kuwahudumia. Tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora za Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano kwa lengo la kukuza maendeleo ya nchi yetu na kanda ya Afrika Mashariki,” amesema .

Amesema Serikali imeonesha dhamira thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo ya nchi.

Amesema malengo ya serikali hadi kufikia 2025, Mkongo wa Taifa uwe umefikia Km 15,000 umeunganisha mikoa na wilaya zote,” alisema na kuongeza kuwa upanuzi wa Mkongo wa Taifa ni mojawapo ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali katika sekta hiyo na unatarajiwa kuleta faida nyingi kwa wananchi wa Tanzania ikiwa
pamoja na; kuimarisha uchumi, kuboresha, kuiunganisha na kuongeza ushindani wa kimataifa.

Kadhalika aliitaka TTCL kuhakikisha BBS wanapata huduma bora na yenye uhakika kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliosainiwa kati ya pande zote mbili.

Amesema hiyo ni muhimu kwa sababu BBS inategemea sana huduma za TTCL ili kuendesha
shughuli zao kwa ufanisi.

Amesema mkataba unaleta fursa nyingi za kibiashara kwa mabenki, mitandao ya simu, na makampuni mengine yaliyopo Tanzania na kuyaomba mabenki, mitandao ya simu, na makampuni mengine kuchangamkia fursa hiyo ya mkongo.

Mtendaji Mkuu wa BBS, Hageringwe amesema ni mkataba wenye kuleta manufaa baina ya nchi zote mbili na pia utatoa huduma rafiki na bora Kwa wananchi wa Burundi.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Peter Ulanga amesema mkongo wa Taifa umeleta mabadiliko katika sekta mbalimbali za uchumi,biashara,jamii na usalama katika ukanda wa Afrika Masharika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button