Bwawa na Kidunda tiba ya kudumu maji Dar

UTEKELEZAJI wa mradi wa Bwawa la Kidunda wenye thamani ya Sh bilioni 329 utakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kwa miaka mitatu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia serikali imeanza kutekeleza mradi wa maji kutoka Mto Rufiji kwenda Dar es Salaam utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 750 kwa siku.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Cyprian Luhemeja alisema jana kuwa mradi wa Kidunda ulisanifiwa mwaka 1951 wakati unajengwa mtambo wa Mtoni na wakati huo pia mchakato wa kujenga mtambo wa Ruvu Juu ulianza na kukamilika mwaka 1959.

Luhemeja aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa mchakato wa mradi wa mtambo wa Ruvu chini ulianza kati ya mwaka 1968-1969 na ukakamilika mwaka 1975 lakini wakati Ruvu chini inajengwa Kidunda haikujengwa, hivyo Ruvu chini na Ruvu juu zilikuwa zinaleta maji Dar es Salaam kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

“Tunamshukuru Mama Samia kwa sababu mradi huu sasa utajengwa kwa muda mfupi kwa miaka mitatu na unajengwa kwa kutumia fedha ya ndani na siyo fedha ya wafadhili,” alisema.

Luhemeja alisema mradi huo utakapokamilika, utasaidia mtambo wa Ruvu Chini na Ruvu Juu kuzalisha maji wakati wote mwaka mzima.

Alisema mpango wa kuongeza pampu moja Ruvu Chini utaongeza uwezo wa kuzalisha lita milioni 360 kutoka lita milioni 270 za sasa ifikapo Juni mwakani na kufanya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa pamoja kuzalisha lita milioni 515 za maji.

“Kwa hiyo kwa bwawa la Kidunda, maji yatakuwepo muda wote na uwezo wa Kidunda ni kuhifadhi maji kwa miaka mitatu mvua zikiwa hazinyeshi, yaani mvua zikikoma kwa miaka mitatu bado tutakuwa salama,” alisema Luhemeja.

Alisema Rais Samia pia ameridhia kujengwa kwa mradi mpya wa maji Mto Rufiji na tayari mhandisi mshauri yuko eneo la mradi akifanya usanifu wa bomba na tangi la maji litakalojengwa Kisarawe.

Luhemeja alisema mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 750 kwa siku, hivyo baada ya miaka mitatu ijayo, Dar es Salaam itakuwa na maji mengi na itakuwa salama kwa miaka 50 ijayo.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 umeweka kipaumbele katika upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama vijijini na mijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Mpango umelenga kuhakikisha asilimia 95 ya idadi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam na makao makuu ya mikoa wanapata maji ya bomba au maji yanayolindwa kama chanzo kikuu.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeielekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mijini inakuwa asilimia 95 na vijijini inakuwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Habari Zifananazo

Back to top button