Byabato awafariji yatima Bukoba Mjini

MBUNGE wa Jimbo la Bukoba Mjini, Wakili Stephen Byabato kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamewakutanisha watoto yatima 200 wanaoishi Manispaa ya Bukoba na kuwapa mahitaji muhimu ya shule, vyakula na mahitaji binafsi kuelekea mwisho wa mwaka.

Tamasha hilo limefanyika jana kwa jitihada za wadau waliopo Kundi Songezi (WhatsApp Group) la Bukoba Mjini Mpya chini ya ulezi wa Byabato na wadau nje ya kundi hilo.

Katika maandalizi ya tamasha hilo, zaidi ya Sh milioni 10 zilitolewa na wadau na kukabidhi sadaka mbalimbali kwa watoto yatima zikiambatana na tuzo za utambuzi kwa waanzilishi na vyeti vya shukrani kwa wasimamizi wa vituo hivyo.

Pamoja na zawadi nyingi zilizotolewa zikiwemo za sikukuu, vimetolewa pia vitabu vya dini (Biblia na Quran Takatifu) yametolewa madawati 50 kwa shule za msingi zenye uhitaji zaidi za Byabato, Bilele, Rwamishenye na Bunena.

Aidha katika kuunga jitihada za Mbunge Byabato, mdau kutoka Afrika Kusini, Injinia Datusi, ametoa vitanda 20 kwa watoto yatima, huku wafanyabiashara wa Soko Kuu Bukoba na wadau wengine wakitoa zawadi mbalimbali kwa watoto hao, TRA Kagera wakakamilisha furaha kwa kuwalisha wahudhuriaji wote zaidi ya 500 chakula cha pamoja cha kiwango cha juu.

Mbunge Byabato kakamilisha tamasha hilo kwa kuwaalika wana Bukoba wote katika tamasha kubwa la Mkoa wa Kagera chini ya uanzilishi na usimamizi wa Mkuu wa Mkoa, Hajjat Fatma Mwassa kuanzia kesho.

Wadau mbalimbali wamepongeza ubunifu, mafanikio na majitoleo hayo yaliyoratibiwa vema na Kamati ya Maandalizi. Wameomba tamasha hili liwe endelevu kwa ajili ya kuwaleta pamoja watu wote.

Habari Zifananazo

Back to top button