MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameshauri Ofisi ya Rais TAMISEMI ichukue hatua kwa watumishi wanaodaiwa kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha za umma.
Ripoti ya CAG imeonesha kuwepo kwa vikundi 48 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopewa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 895.94 kwenye Mamlaka tatu za Serikali za Mitaa huku Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na vikundi hewa 34 vilivyokopeshwa Sh milioni 698.7.
Kichere ameyabainisha hayo jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa za ukaguzi bungeni kwa hesabu za mwaka 2021/22.
Alisema katika ukaguzi huo walibaini kuwa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata husika hawakufahamu lolote kuhusu vikundi hivyo ikiashiria matumizi mabaya ya fedha za umma.
Aidha, Kichere alisema kupitia ukaguzi huo, alibaini kuwa Mamlaka kadhaa za Serikali za Mitaa hazikuweza kukusanya mikopo iliyotolewa kwenye vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu yenye thamani ya Sh bilioni 88.42.
Alisema kuwa tathmini ilibaini kuwa, mamlaka tisa za serikali za mitaa zilikuwa zikitoa mikopo ambayo haijakurejeshwa yenye Sh bilioni 2.25 kutoka kwenye vikundi 627 vilivyositisha shughuli zao za biashara.
Taarifa hiyo inaonesha Halmashauri ya Geita inaongoza kwa kuwa na vikundi 396 na fedha zilizokopwa takribani Sh bilioni 1.055.
Pia mamlaka 53 za serikali za mitaa zilishindwa kuchangia Sh bilioni 5.06 kwenye mfuko wa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kutoka katika vyanzo vyao vya mapato kinyume na sheria.
Kichere alisema pia ukaguzi umebaini kuwa bado kuna changamoto ya fedha mbichi kuliwa kwenye baadhi ya halmashauri nchini huku akipendekeza kuwekwa sera za udhibiti zikiwemo za makubaliano kati ya halmashauri na watumiaji wa POS.
“Ninapendekeza kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI ifanye mapitio ya taratibu za kuwasilisha benki mapato yanayokusanywa kupitia POS na kuweka sera za udhibiti zikiwemo za makubaliano kati ya Halmashauri na watumiaji wa POS juu ya uzingatiaji wa muda wa kuwasilisha makusanyo benki na utozaji wa faini kwa ucheleweshaji ili kuhakikisha fedha zinawasilishwa benki kwa wakati.”alisema na kuongoza;
“Ninasisitiza Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha kwamba fedha ambazo hazikuwasilishwa benki zinarejeshwa.”
Kichere alisema mwaka 2021/2022 mapato ya ndani yaliyokusanywa na halmashauri 184 yalikuwa Sh bilioni 891.84 ambayo yalivuka makadirio ya bajeti kwa asilimia 102.
Kichere alisema katika tathimini ya taarifa za mfumo wa mapato (LGRCIS) alibaini kuwa mapato ya Sh bilioni 11.07 hayakupelekwa kwenye akaunti za benki za mamlaka za serikali za mitaa husika.
Pia mapato ya Sh bilioni 76.59 hayakukusanywa hususani yatokanayo na tozo za vizimba vya masoko, uuzaji wa viwanja, mazao ya kilimo, leseni za vileo, ushuru wa uchimbaji wa vifaa vya ujenzi, leseni ya biashara, ushuru wa huduma, kupangisha maduka ya nyumba zilizopo katika stendi ya mabasi na masoko ya halmashauri.
Pia Sh bilioni 13.15 ambazo hazikuwa zimekusanywa kutoka kwa wadaiwa waliopewa hati za madai za mfumo wa mapato (LGRCIS) bila kubainisha sababu.
Kichere alisema Sh bilioni 4.94 hazikuwasilishwa na mawakala wa ukusanyaji mapato kulingana na makubaliano ya mikataba.
Alisema ukaguzi wake umebaini kuwa miradi yenye thamani ya Sh bilioni 20.29 ilitekelezwa na wakandarasi ambao dhamana zao za utendaji kazi zilikuwa zimeisha.
Alisema pia malipo ya awali ya Sh bilioni 1.83 yaliyofanywa kwa mkandarasi hayakurejeshwa, wakati dhamana ilikuwa imeisha muda wake hadi kufikia tarehe ya ukaguzi huu.