CBT, vyama vya ushirika kuuza mazao

BENKI ya Ushirika Nchini (CBT) kwa kushirikiana na vyama vikuu vya ushirika Lindi, Mtwara na Songea kwa mara ya kwanza itasimamia na kutoa malipo ya mazao ya ufuta ,mbaazi na mazao mengine ya biashara kutoka mikoa ya kusini katika msimu wa mauzo 2025/2026.
Mkurungezi Mtendaji wa Benki hiyo Godfrey Ngu’rah amesema hayo mkoani Mtwara wakati wa kikao kilichokutanisha watendaji wa benki na viongozi wa vyama vya ushirika.

“Benki ya Ushirika tumejipanga, tumeweka miundombinu ya huduma zote kuwezesha malipo kwenda kwa wakulima kwa haraka sana,” amesema.
Ngu’rah amesema benki imewezesha vyama vikuu vya ushirika kupitia benki hiyo kufanya malipo moja kwa moja kwenda kwenye akaunti za wakulima kwa njia ya mtandao (internet banking).
Godfrey amesema hatua hiyo imelenga kurahisha malipo ya wakulima na kuondokana na changamoto ambayo ilikuwa ikichelewesha malipo ya wakulima.

Amesema benki hiyo imewezesha watendaji wa vyama vya ushirika kuwa kama mawakala wa Benki kutumia teknolojia kutoa malipo kwa wakulima.
“Tumewezesha vyama vya ushirika kama mawakala, vitafungua akaunti ya wanachama wake, kupokea na kutoa na kulipa fedha kwa wakulima wao,” amesema.
Msimu wa uuzwaji wa ufuta 2025/2026 unatarajiwa kuanzia Juni 13, 2025 katika mkoa wa Mtwara.



