CCM kuamua wagombea ubunge kesho

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, Rais Samia alieleza kuwa vikao hivyo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya chama kupata wagombea ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wengine ni wabunge wa viti maalumu, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe wa baraza la wawakilishi viti maalumu.
Rais Samia alieleza CCM itateua wagombea hao kabla ya uteuzi wa mwisho utakaofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kisha kwenda kuomba ridhaa ya wananchi kwa kampeni za uchaguzi mkuu.
Viongozi mbalimbali wakuu wa CCM walihudhuria kikao cha jana akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.
CCM imemaliza michakato ya awali ya kupata wagombea wa majimbo 272 na ubunge viti maalumu na kesho kutakuwa na kikao cha mwisho cha kufanya uamuzi.
Taarifa iliyotolewa Agosti 17, mwaka huu na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ilieleza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kitafuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kesho.
Vikao hivyo vitateua wagombea ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabunge wa viti maalumu.
Pia, vitateua wagombea ubunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe wa baraza la wawakilishi viti maalumu.
Wagombea kupitia majimbo watapigiwa kura kwenye majimbo 272 yakiwemo 222 ya Tanzania Bara na 50 ya Tanzania Zanzibar.
Tanzania bara kuna majimbo manane mapya.



