CCM Mbeya yawakumbusha viongozi wajibu

MBEYA: MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amewataka viongozi wa chama hicho kuwatumikia wananchi ipasavyo ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake katika maeneo yao.

Amesema uongozi walionao umetokana na imani ya wananchi kwa kuwachagua ili waweze kuwawaikilisha vyema katika Serikali Kuu na kuwaletea maendeleo katika maeneo yao pamoja na kuwatatulia changamoto zao.

Akizungumza na wenyeviti wa mtaa, makatibu Kata na Madiwani jijini Mbeya leo, Mwalunenge amesema ni vyema kila mmoja akatambua wajibu wake katika kuwatumikia wananchi bila kuangalia hali walizonazo.

Advertisement

“Mkawatumikie watu bila kubagua na bila kuchagua huyu ana uwezo au hana uwezo, nikigundua hayo yanafanyika unanyanyasa watu na hutatui changamoto zao, kwa sababu sisi kama chama ndiyo tuliokupa dhamana, hatutasita kukusimamisha na hilo naongea wazi kweupe.

Ombi letu kwenu kama chama ni kwenda kufanya kazi kwa ajili ya wananchi bila kuchoka na bila kujali masaa ya kazi ili wananchi waone kupanga kwao foleni na kukupigia kura kuna thamani”, alisema Mwalunenga.