CCM yaahidi kufanya makubwa

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi zinazolenga kujenga taifa lenye ustawi na kujitegemea kwa kuimarisha huduma za kijamii na kuchochea shughuli za kiuchumi katika kilimo, ufugaji, viwanda na biashara.

Samia alitoa ahadi hizo katika siku nne za mikutano ya kampeni ukiwemo uzinduzi mkoani Dar es Salaam na kwenye majimbo ya uchaguzi kwa mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Aliahidi kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuongeza shule mpya za msingi, sekondari na nyumba za walimu kutokana na kuwepo mahitaji.

Samia aliahidi kujenga vituo vipya vya afya na zahanati ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kujenga njia ya kusafirishia umeme ya kilovoti 220 kutoka Morogoro kwenda Dumila na kilovoti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma.

“Natambua uwepo wa ongezeko la idadi ya watu, kwa hiyo bado kuna haja ya kuimarisha huduma za kijamii kwa kujenga shule na vituo vya afya zaidi ili kukidhi mahitaji,” alisema.

Rais Samia pia aliahidi kuanzisha kongani za viwanda, kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo cha kisasa, kujenga vituo vya zana za kilimo, kununua trekta 10,000, kujenga maghala ya kuhifadhia mazao na kuimarisha miundombinu ya barabara ili zipitike muda wote.

Akifanya kampeni Kata ya Ngerengere mkoani Morogoro, Rais Samia alisema chama chake kikipewa ridhaa na wananchi, serikali itajenga vituo vya zana za kilimo katika maeneo ya kilimo vitakavyotoa huduma za ukodishaji trekta kwa gharama nafuu ikiwa ni nusu bei inayotozwa na watu binafsi.

Pia, itajenga maghala mawili ya kuhifadhia mazao na kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuwa ushoroba wa viwanda  vitakavyochochea ukuaji wa uchumi.

Mbali na kuendelea kuwapatia wakulima ruzuku ya mbolea, serikali itaanzisha kituo cha uzalishaji miche ya michikichi na kuahidi kujengwa barabara ya Bigwa-Mvuha-Kisaki kwa kiwango cha lami.

Katika mkutano wa kampeni, Morogoro Mjini, alibainisha mambo ambayo CCM imepanga kuyafanya ndani ya miaka mitano ijayo baada ya kupewa ridhaa na wananchi kuwa ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama kuongeza uwezo wa Bwawa la Mindu na kuboresha mtandao wa barabara za pembezoni, za mjini na madaraja ili yapitike muda wote ikiwamo barabara ya Ifakara- Mahenge kwa kiwango cha lami.

 

Aliahidi pia kuufungua Mkoa wa Morogoro kwa viwanda, biashara na utalii na kujenga kituo kikubwa cha mikutano.

Rais Samia aliahidi kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya kwa kujenga  vituo vya afya viwili na zahanati 11 na kujenga wodi ya mama na mtoto na jengo la upasuaji.

Tutaendelea pia kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya za msingi na sekondari kulingana na mahitaji.

Rais Samia aliahidi kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea ya ruzuku, mbegu bora na ujenzi wa vituo vya zana za kilimo ili kumpungizia mkulima gharama na kujenga masoko ya kisasa Morogoro Mjini na Wilaya ya Malinyi.

Akiomba kura Jimbo la Mvomero, Rais Samia aliahidi kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Dakawa na kujenga zahanati katika Kijiji cha Njeula.

Pia, kujenga na kuboresha shule za sekondari katika Kata za Chenzema, Pemba, Mkindo, Dakawa na Homboza na kukamilisha vyumba vya madarasa 31 katika shule za msingi.

Rais Samia pia aliahidi kujenga machinjio ya kisasa eneo la Mhando na Mkongeni na kujenga njia ya kusafirishia umeme kilovoti 220 kuanzia Morogoro hadi Dumila.

Akiwa katika Jimbo la Kilosa, Rais Samia aliahidi kutatua changamoto ya maji kwa kutekeleza miradi mkubwa na kuendelea na utoaji wa huduma ya elimu na afya kwa kujenga shule za msingi, sekondari na vituo vya kutolea huduma ya afya ili kukidhi mahitaji.

Pia, kuongeza maeneo ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.46 hadi ekari milioni sita na kuongeza kasi ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi hatua itakayoondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Rais Samia pia aliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami barabara ya Kilosa-Ulaya-Mikumi, kujenga soko la kisasa na kuendelea na utoaji wa ruzuku kwenye mbolea, pembejeo na zana za kilimo na kukamilisha mradi wa Bwawa la Kidete litakalotumika kwa shughuli za kiuchumi.

Akieleza sera za CCM kwa wananchi wa Jimbo la Gailo, Rais Samia aliahidi kujenga soko la kisasa la Rubeho.

Pia, kuongeza vituo vya afya vitano na zahanati 11, kujenga Chuo cha Veta cha Wilaya ya Gairo na kujenga machinjio ya kisasa kata nne za Leshata, Iyogwe, Kibendya na Italangwe.

 

Aidha, akiwa eneo la Kibaigwa, Rais Samia aliahidi ujenzi wa vituo vya afya 10 na zahanati 21 katika Jimbo la Kongwa.

Pia, kuanzisha minada 10 ya mifugo, majosho 35 na machinjio manne ili kuimarisha kilimo na ufugaji na kuhakikisha vitongoji vyote vinaunganishwa na nishati ya umeme, na kujenga shule mpya ikiwemo Sekondari ya Kibaigwa.

Akiwasalimia wananchi wa Chamwino, Rais Samia aliahidi kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo kwa ajili ya vijana.

Pia, kutatua changamoto ya maji na kuimarisha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya 10 na zahanati 5 na kuimarisha barabara.

Akiomba kura Jimbo la Chemba, Rais Samia aliahidi kununua zana za kilimo ikiwemo matrekta 10,000 ambayo yatakodishwa kwa bei nafuu na zana zingine za kilimo.

Pia, aliahidi kuanzisha kongani ya viwanda na kuimarisha barabara za jimbo hilo ikiwamo kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara za Chemba – Soya ambayo imekuwa ikilalamikiwa muda mrefu.

Kuhusu barabara ya Kwamotoro – Mpende – Kasakai – Ilahoda na zingine tatu za ndani ya wilaya hiyo, aliahidi kuangalia uwezekano Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuiboresha ili itumike katika kipindi chote.

Pia, aliahidi kutimiza ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli ya kujenga soko na stendi ndani ya Mji wa Chemba.

Akiomba ridhaa ya wananchi wa Kondoa, Rais Samia aliahidi kuboresha mazingira ya biashara kwa kutenga maeneo ya biashara na uwekezaji na kujenga soko la kisasa.

Samia aliahidi kumaliza changamoto ya maji, kujenga vituo vya afya vipya vinne na zahanati tano na kukamilisha ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya ambayo ujenzi wake uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Alisema pia kutokana na uwepo wa mahitaji ya madarasa, serikali yake itakwenda kuongeza shule mpya za msingi na sekondari na nyumba za walimu ili watoto wa kitanzania wapate elimu katika mazingira bora ya ujifunzaji na ufundishaji.

Kwenye miundombinu, alisema serikali yake itajenga madaraja na kuimarisha barabara ili ziweze kupitika muda wote.

Aliahidi pia kuanzisha mashamba ya kilimo cha kisasa na kukamilisha mradi wa skimu ya umwagiliaji ya hekta 150 ili wakulima walime mara mbili kwa mwaka.

Akiwa Dodoma Mjini, Rais Samia aliahidi neema kwa wanaDodoma ikiwa ni pamoja na kumaliza tatizo la maji kwa kutekeleza mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria na kujenga Bwawa la Farkwa.

“Kwa sababu Dodoma ni makao makuu ya nchi, si vyema kuwa na shida ya maji kwa hiyo tunakwenda kumaliza kabisa shida ya maji kupitia mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria na kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa,” alisema.

Alisema pia atamaliza changamoto ya umeme kwa kujenga njia ya umeme ya kilovoti 400 kitoka Chalinze hadi Dodoma na kukamilisha Uwanja wa Ndege wa Msalato na kujenga uwanja mkubwa wa mpira.

Rais Samia aliahidi kuvutia wawekezaji kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na pia alitoa ahadi ya kuongeza kasi ya upimaji na usajili ardhi ili kutatua migogoro.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Google paid $220 an hour on the internet. My close relative has been without labor for nine months and the earlier month her compensation check was 25k by working at home for 10 hours a day….. Everybody must try this job now by just use this link

    COPY THIS→→→→ http://Www.CartBlinks.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button