CCM yafunika Dar, Samia aahidi makubwa siku 100 ofisini

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kufanya makubwa katika siku 100 akichaguliwa kuiongoza nchi kwa miaka mitano ijayo zikiwemo ajira 12,000 katika sekta za afya na elimu.
Alisema serikali atakayoiunda itazingatia mabadiliko yenye kugusa maslahi ya mwananchi moja kwa moja katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Samia alisema hayo alipozungumza na maelfu ya wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Alisema pia serikali yake itapiga marufuku hospitali kuzuia miili ya marehemu.
“Tutapiga marufuku hospitali kuzuia miili ya marehemu kuchukuliwa kwa sababu ya kudaiwa gharama za matibabu, tutakachofanya ni kuja na mfumo mwingine wa kuhakikisha jamaa wa marehemu wanalipa gharama lakini siyo kuzuia miili,” alisema Samia.
Aliongeza: “Kupitia Bima ya Afya kwa Wote tutazindua mfumo wa mfumo wa taifa kwa awamu ya majaribio kuanzia wazee, wototo, wajawazito ambapo gharama za matibabu zitabebwa kupitia mfuko wa bima ya afya. Pia serikali itagharamia kwa asilimia 100 wananchi wasiokuwa na uwezo kupata vipimo vya figo, moyo, sukari, mishipa ya fahamu na mifupa”.
Samia alisema ndani ya siku 100 serikali yake itatoa ajira 5,000 katika sekta ya afya wakiwemo wauguzi na wakunga ili kuimarisha utoaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto.
Rais Samia alisema pia muda huo serikali yake itaweka mkakati wa elimu kisayansi ambao kila mtoto wa darasa la tatu awe na uwezo wa kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida na itaajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi.

“Pia tutazindua mpango wa pamoja utakaohusisha waajiri, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele, lengo ni kuwafanya wanafunzi wa VETA kuchukuliwa viwandani kufanya kazi za mazoezi kwa vitendo,” alisema.
Samia alisema pia serikali yake itatenga Sh bilioni 200 za kuwezesha upatikanaji mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na kati, uanzishwaji kampuni changa, kurasimisha wajasiriamali wadogo wakiwemo bodaboda, mama lishe, wafanyabiashara wadogo kuingizwa katika mfumo rasmi wa serikali.
Alisema serikali itaanzisha programu ya mitaa ya viwanda wilayani kwa lengo la kuzalisha ajira kupitia mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi madini na misitu.
Samia pia alisema katika kipindi hicho serikali itakayoiunda itaanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji ili kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji ambayo pia itahusisha vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa na mito mikubwa.
Ahadi nyingine aliyoitoa ni kuendeleza jitihada nishati safi kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuweka mifumo rafiki ya uwajibikaji kwa mawaziri na wakuu wa mikoa kutakiwa kutoa taarifa na kujibu maswali kwa wananchi kwa njia ya simu.
Samia alisema serikali itaendelea na mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi ikiwemo kuunda tume maalumu ya kuandaa mazingira ya mchakato wa katiba mpya.

Alisema amegombea uraia kwa kuwa serikali imefanya vyema na kufanikiwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na pia chama hicho kinaamini uwezo wake katika kulitumikia Taifa.
Samia alitaja mafanikio yaliyopatikana na kupitia falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) Tanzania inaongoza kwa amani na utulivu kwa mujibu wa ripoti za kimataifa Afrika Mashariki.
Alisema wakati anaingia madarakani alikuta changamoto ya uhuru wa vyombo vya habari na aliweka wazi utashi wa kisiasa na misingi ya kisheria kwa kuondoa kifungoni magazeti yaliyofungiwa, kuboresha sheria ya habari, kutoa leseni zaidi ya 1,000 kwa magazeti, redio zaidi ya 200, mitandao ya kijamii zaidi ya 300 na blogu zaidi ya 70.
Rais Samia alisema serikali imefanikiwa kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alisema hatua hiyo imewezesha Tanzania kushika nafasi ya 82 kutoka nafasi ya 87 kati ya nchi 170 zilizofanyiwa tathmini duniani.
Kwa upande wa hati chafu, alisema mwaka 2021 zilikuwa 10 huku zenye mashaka zikiwa 81 lakini kwa mwaka jana hati chafu ilikuwa moja na zenye mashaka zilikuwa hati tano.
“Bajeti ya serikali imeongezeka kutoka Sh trilioni 34.9 hadi Sh trilioni 59.49 mwaka huu, deni la taifa hadi mwaka jana kwa serikali zote duniani lilikuwa asilimia 93 ya pato la dunia, wakati deni la serikali kwa nchi za Afrika lilikuwa asilimia 67 ya pato lote, Afrika Mashariki lilikuwa asilimia 67 kwa wastani wa nchi zote.
“Tanzania lilisalia asilimia 46 ya Pato la Taifa. Ni kiwango kidogo ukilinganisha na wastani wa asilimaia 67,” alisema.
Kwa upande wa sekta ya madini, Rais Samia alisema serikali ilisambaza mitambo kwa wachimbaji wadogo ambayo imesaidia mchango wa wachimbaji hao kutoka asilimia 20 hadi asilimia 40 kwa mwaka jana.
Alisema uzalishaji almasi umeongezeka kwa karati 213,948 hadi 373,252.76 mwaka jana, viwanda vya uchakataji madini vimetoka kuwa viwili hadi kufikia tisa.
Akizungumzia utalii, alisema idadi ya watalii wa ndani na nje imefikia milioni 5.3 kutoka milioni 1.4 mwaka 2020, mawakala wa biashara za utalii wameongezeka kutoka 2,885 hadi zaidi ya 3,000 mwaka huu huku mapato ya utalii yakiongezeka kutoka dola milioni 700 hadi dola bilioni 3.9 mwaka jana.
Kuhusu upatikanaji wa mbolea, alisema umeongezeka kutoka tani 600,000 hadi tani milioni 1.4 mwaka jana ambapo serikali imetoa ruzuku ya Sh bilioni 708.
“Tulikuwa tunauza mazao ya biashara, sasa tunauza mbaazi, mahindi, mchele. Serikali kupitia benki ya kilimo imewezesha upatikanaji mikopo nafuu ya riba isiyozidi asilimia tisa,” alisema.
Aliongeza: “Mauzo ya mazao kupitia minada ya kimataifa yameongeza kutoka thamani ya Sh trilioni 1.1 hadi Sh trilioni 4.2 mwaka huu.”
Rais Samia alisema mauzo ya mazao nje ya nchi yamefikia Sh trilioni 9.2 kutoka Sh trilioni tatu kwa mwaka 2020.
Akizungumzia mafanikio ya reli ya SGR alisema utekelezaji mradi huo kwa Dar es Salaam hadi Morogoro tayari umeshakamilika, kipande cha SGR kuingia bandarini kimefikia asilimia 91.7 kwa lengo la kurahisisha usafirishaji mizigo.
Pia, alisema ujenzi wa SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora umefikia asilimia 97.9, Makutupora – Tabora (asilimia 14.5) Tabora – Isaka (asilimia 6.5) Mwanza – Isaka (asilimia 63.1) Tabora – Kigoma (asilimia nane).
Alisema kukamilika kwa vipande hivyo, kutaimarisha biashara kati ya nchi jirani.
Vilevile, alisema ujenzi huo umetengeneza ajira zaidi ya 9,000 huku serikali ikinunua mabehewa 264 ya mizigo.
Aidha, alisema serikali imeingia makubaliano na Zambia kuboresha Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kupitia mkataba wenye thamani Dola za Marekani bilioni 1.4.
Rais Samia alisema kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, imeongeza uwezo kuhudumia mizigo kutoka tani milioni 17 hadi tani milioni 27, muda wa kutia nanga umepungua.



