CCM yaipa tano Ruwasa mfumo wa kulipia maji

CHAMA Cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe kimetoa pongezi kwa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kufunga mfumo wa kulipia maji kwa njia ya kadi jambo ambalo limeokoa upotevu wa mapato na maji.

Kamati ya siasa chini ya mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Paschale Rwamugata wametembelea mradi wa maji wa Nyakahiga na kushangazwa namna wananchi wanavyolipia maji kwa wakala kupitia kadi.

Rwamugata alisema mfumo huo kama utatumika katika miradi yote ya maji ndani ya wilaya basi hakuna mradi ambao utashindwa kujiendesha na hakutakuwa na upotevu wa maji kwani ukiweka kadi ujazo wa maji unaishia kwa kiwango ulicholipia  na hakuna maji yanayomwagika wala kuibiwa.

“Kama teknolojia hii inaweza kufungwa katika vituo vyetu vyote vya miradi hakuna mradi utaacha kufanya kazi ,kwa sababu changamoto kubwa ni wananchi kuchangia gharama za uendeshaji lakini katika mradi huu wa Nyakaiga tunaona unapata maji kwa jinsi ulivojaza katika kadi yako , hii ni hatua njema. “alisema Rwamugata.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Karagwe Cassian Wittike alisema kuwa kabla ya kufunga mfumo huo makusanyo ya miezi mitatu ya mauzo ya gharama za wananchi kulipia huduma za maji ilikiwani kiasi cha Sh milioni 8 lakini baada ya kufunga mfumo huo makusanyo ya gharama za wananchi ndani ya miezi mitatu ni milioni 20 .

Alisema mfumo huo ulitumia kiasi Sh milioni 36  kuufunga na kukamilisha kila kitu hivyo kwa sasa hakuna haja ya mlinzi katika kituo cha kuchotea maji na tayari kadi 500 zipo wananchi wanajaziwa pesa zao na kila ukichukua maji bombani mfumo unakuonyesha salio lako la kununua maji katika kadi yako.

Habari Zifananazo

Back to top button