CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejivunia utekelezaji wa mikakati ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuboresha vyama vya ushirika, miundombinu ya umwagiliaji na upatikanaji wa pembejeo.
Hayo yalielezwa jana Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kuanzia Novemba 2020 hadi Desemba 2024.
Alisema serikali imeimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka 2,150 mwaka 2020 hadi 4,060 mwaka 2024 na kuchangia mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika ambayo iko katika hatua za mwisho, ikiwemo kufikia lengo la ukwasi wa Sh bilioni 50.
“Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 18.6 mwaka 2020 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2024. Uzalishaji huo ulichagizwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbolea kwa asilimia 107 kutoka tani 586,604 mwaka 2020 hadi tani 1,213,729 mwaka 2024,” alieleza Majaliwa.
Pia, alisema mbegu bora 46 zimegunduliwa na kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Mbegu ikiwemo za mtama, viazi vitamu na karanga. Vilevile, aina 11 za mbegu na miche bora ya chikichi, migomba, mihogo, minazi na pareto zimegunduliwa na mafunzo kuhusu matumizi ya mbegu bora yametolewa kwa wadau 2,034,859.
Kwa upande wa viwanda taarifa hiyo ilibainisha vimeanzishwa viwanda vya sekta binafsi ikiwemo kiwanda cha sukari cha Bagamoyo chenye uwezo wa kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa mwaka na kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na ajira 9,000 zisizo za moja kwa moja. Viwanda vipya vilivyoanzishwa ni kiwanda cha ndege Morogoro (Airplanes Africa Ltd) na Sapphire Float Glass kinachozalisha tani 700 za vioo kwa siku.
“Kuhamasisha uanzishaji wa viwanda 12 vya sekta binafsi ambapo viwanda vitatu ni kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za binadamu na viwanda tisa ni kwa ajili ya uzalishaji wa vifaa tiba na vitendanishi, kuwezesha upatikanaji wa masoko ya nje ya nchi kama vile maonesho ya Dubai EXPO 2020 yaliyowezesha Tanzania kusaini makubaliano ya miradi ya thamani ya Dola bilioni 7.49 na kuwezesha uuzwaji wa aina 10 za mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani,” alieleza Majaliwa katika taarifa hiyo.
Kwa upande wa uvuvi taarifa ilibainisha kuwa uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita bilioni 3.1 mwaka 2020 hadi lita bilioni 3.97 mwaka 2024 kulikochagizwa na ongezeko la ng’ombe wa maziwa kutoka milioni 1.2 hadi milioni 1.4 mwaka 2024. “Serikali imefanikiwa kutoa mafunzo kwa vijana 240 katika vituo nane vilivyoanzishwa kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kuimarika kwa huduma za ugani kwa kuajiri maofisa 764 wa huduma za ugani katika serikali za mitaa na kutoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji 47,643 ili kusaidia kuongeza tija kwenye mifugo,” ilifafanua taarifa hiyo.