CCM yakana kusaidia mgombea Chadema

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amekanusha madai kuwa chama hicho kimetoa fedha kwa ajili ya kusaidia kambi mojawapo ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kushinda.

Hivi karibuni ziliibuka tuhuma kuwa CCM kinaingilia uchaguzi wa ndani wa Chadema na kwamba kimesimama na mgombea mmoja anayewania kiti cha uenyekiti wa chama taifa kwa kumsaidia kifedha na kiulinzi.

Makalla alikanusha tuhuma hizo jana mkoani Dodoma alipoulizwa na mtangazaji wa Kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha UTV kuhusu madai kuwa CCM kinaingilia uchaguzi wa ndani wa Chadema.

Alisema tuhuma hizo alizisikia katika vyombo vya habari na kwamba chama hakijapata malalamiko hayo na kuweka wazi kuwa CCM hakijawahi kujihusisha kwa vyovyote katika uchaguzi huo unaoendelea ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

“Tuhuma hizi hata sisi tumezisikia tu katika vyombo vya habari lakini ni tuhuma ambazo hazina uhalisia wowote na hatuna sababu yoyote ya kuingilia uchaguzi huo unaoendelea mpaka sasa,” alisema Makalla.

Alisema CCM hakiwezi na wala hakitathubutu kujihusisha na fedha chafu na kwamba kama kuna ushahidi ni bora walalamikaji wakaenda mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Hii si mara ya kwanza Chadema kukilalamikia CCM kuwa kinatoa fedha chafu kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi wa chama hicho.

Mwishoni mwa mwaka jana aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu alisema kuna fedha chafu nyingi zimemwagwa kwa baadhi ya viongozi wa chama wakati wa kufanya chaguzi za kanda mbalimbali za chama.

Lissu ambaye kwa sasa ni mmoja wa wagombea ngazi ya Mwenyekiti Taifa akichuana na Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe alisema baadhi ya viongozi wa juu wa chama wanahusika na fedha hizo akisema zimelenga kukisambaratisha chama.

Kuhusu mchakato wa kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030, alisema mchakato umekamilika kwa asilimia kubwa na kitabu kitatoka baada ya ilani ya sasa kufikia ukingoni.

 

Habari Zifananazo

Back to top button