CCM yakosa upinzani ubunge Mvomero, Ngorongoro

WAGOMBEA ubunge katika majimbo ya Mvomero mkoani Morogoro na Ngorongoro mkoani Arusha wamekosa wapinzani.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemteua Sarah Msafiri kuwa mgombea pekee wa ubunge Mvomero kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wagombea wanane walichukua fomu za kuomba uteuzi kwa msimamzi wa uchaguzi wa Jimbo la Mvomero, Mary Kayowa.

Mary amesema kuwa wagombea walioomba uteuzi walikuwa wa vyama vya Alliance for Democratic Change (ADC), Tanzania Labour Party (TLP) na United Democratic Party (UDP), Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Makini, National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha Wananchi (CUF) na CCM lakini wa CCM pekee alikidhi masharti.

SOMA: Majina ya walioteuliwa CCM yanatangazwa

Alisema wagombea kupitia ACT Wazalendo na ADC hawakurudisha fomu na mgombea kupitia UDP fomu zake zilikuwa na upungufu ikiwa ni pamoja na kutokamilisha idadi ya picha na kasoro eneo la udhamini.

Pia, Mary alisema baadhi ya wagombea walichelewa kuwasilisha fomu zihakikiwe katika muda uliopangwa.

Mmoja wa wagombea ambaye hakuteuliwa, Nasra Omar Rajabu wa chama cha NRA alidai fomu zake zilikutwa na dosari katika ujazaji na picha.

Msafiri alitoa mwito kwa wana CCM wavunje makundi ya kura za maoni na waungane ili kuiwezesha CCM ipate ushindi kuanzia urais, wabunge na madiwani.

Kilosa, Mikumi
Msimamizi wa Uchaguzi majimbo ya Kilosa na Mikumi, Joseph Kapere amesema wagombea wanane wameteuliwa kugombea ubunge kwenye majimbo hayo.

Kapere alisema wagombea walioteuliwa Kilosa ni Hassan Mbaruku wa ACT Wazalendo, Silas Kassao wa CUF, Profesa Palamagamba Kabudi wa CCM na David Chiduo wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Alisema walioteuliwa Mikumi ni Dennis Londo wa CCM, Joseph Mdede wa Makini, Kasela Mdachi wa ACT Wazalendo na Imani Mzude wa Chaumma.

Mlimba
Wagombea sita waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Mlimba walirejesha na wameteuliwa.

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Zaituni Kisusi alitaja wagombea walioteuliwa ni Suzan Kiwanga wa Chaumma, Apolinary Ngonga wa ACT Wazalendo na Rakia Utoto wa National League for Democracy (NLD).

Wengine ni Dk Kellen-Rose Rwakatare wa CCM, Ridhiwan Kilala wa African Democratic Alliance Party (ADA TADEA) na Thomas Mchiwa wa National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi).

Ngorongoro
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ngorongoro, Laban Mchome amelieleza HabariLEO mgombea wa ubunge katika jimbo hilo kupitia CCM, Yannick Ndoinyo ameteuliwa mgombea pekee.

Mchome alisema mgombea wa Chaumma, Zakhalia Bayo hakurejesha fomu ya uteuzi katika muda uliopangwa na INEC yaani kabla ya saa 10 jioni juzi.

“Kila mgombea ubunge wakati wa uchukuaji fomu ya ubunge walipewa taratibu zote na nini wanapaswa kufanya ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda uliopangwa na INEC wakati wa urudishaji fomu,” alisema.

Mchome alisema wagombea udiwani kupitia CCM katika kata 26 kati ya 28 wamekosa wapinzani. Alisema kata za Sale na Oldonyosambu wagombea wa CCM walioteuliwa wamepata wapinzani wa chama cha ACT Wazalendo.

INEC imeteua wagombea wa vyama 16 wagombee ubunge Arusha Mjini. Imetaja walioteuliwa ni Paul Makonda wa CCM, Amina Mhina wa ADA TADEA, Simon Bayo wa Sauti ya Umma, Msifuni Mwanga wa TLP na Alfred Mollel wa NLD.

Wengine ni Simon Ngilisho wa Demokrasia Makini, Zuberi Hamiss CUF, Mussa Ayo wa Democratic Party (DP), Mark Diganyeka wa Union for Multiparty Democracy (UMD), Mgina Mustafa wa Alliance for African
Farmers Party (AAFP), Daniel Daffa UDP, Rashid Mkama NRA, Magdalena Masaka wa United Peoples’ Democratic Party (UPDP), Ramadhan Bigo Chama cha Kijamii (CCK), Said Njuki ACT Wazalendo na Benjamin Lema wa Chaumma.

Mgombea kupitia ADC, Shaffii Kitundu alichukua fomu kuomba uteuzi INEC lakini hazikurudishwa.

Longido
Pia, INEC imeteua wagombea ubunge Longido mkoani Arusha akiwemo Dk Stephen Kiruswa wa CCM. Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Nevellng Lyimo ametaja wengine ni Abraham Mzava wa ACT Wazalendo.

Lyimo alisema wagombea wa Chaumma, Ester Makembo na wa TLP, Johnson Mavuma hawakuteuliwa kwa kuwa fomu zoa zilikuwa na kasoro ikiwa ni pamoja na kutopigwa muhuri wa vyama vyao sanjari na kukosa orodha ya malipo ya fomu husika.

Karatu
Katika jimbo la Karatu mgombea ubunge wa CCM, Daniel Awack amepata wapinzani wa vyama vya CCK, Chaumma, Sauti ya Umma (SAU).

Iringa Mjini
Mgombea wa ubunge wa Chaumma, Vitus Nkuna amejitoa kugombea ubunge Iringa Mjini. INEC imeteua wagombea wa vyama saba wakiwemo Fadhili Ngajilo wa CCM na Chiku Abwao wa ACT Wazalendo.

Abwao amewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wengine walioteuliwa ni Ahmed Lyellu wa CUF, Hebron Kileta wa NCCR-Mageuzi, Shukran Mtuli wa DP, Christian Mbalinga wa NRA na Masasi Issa wa ADC.

Bukoba Mjini
INEC imeteua wagombea wanne wa ubunge Bukoba Mjini. Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Melkion Kombo alitaja walioteuliwa ni Johansen Mtasingwa wa CCM, Almasoud Kamala wa ACT Wazalendo, Happiness Mtagaywa wa CUF na Saulo Joseph wa Chaumma.

Moshi Mjini
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Moshi Mjini, Sifael Kulanga alisema wagombea 11 wameteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Alivitaja vyama hivyo kuwa ni CCM, Chaumma, ACT Wazalendo, CUF, Makini, Sau, CCK, NRA, TLP, AAFP na ADC.

Moshi Vijijini
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Moshi Vijijini, Lucas Msele alisema wagombea tisa wameteuliwa kugombea ubunge kwenye jimbo hilo. Msele alisema wagombea hao ni wa vyama vya CCM, Chaumma, CUF, CCK, ADA-TADEA, TLP, NRA, ACT Wazalendo na AAFP.

Vunjo
Msele alisema Vunjo wagombea tisa wa vyama vya CCM, Chaumma, DP, ACT Wazalendo, ADA-TADEA, Makini, CCK, AAFP na TLP wameteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Siha
Msimamizi wa uchaguzi Siha, Marco Masue alisema wagombea sita wameteuliwa kuwania ubunge wa vyama vya CCM, ACT Wazalendo, Makini, Sau, CUF na NRA.

Mwanga
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mwanga, Robert Tarimo amesema wagombea watano walichukua fomu kuomba uteuzi ila watatu kati yao wameteuliwa wakiwa ni wa CCM, ACT Wazalendo na NRA.

Msalala
Msimamizi wa uchaguzi wa Msalala, Abdulkadir Mfilinge amesema wagombea wa vyama sita wameteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Mfilinge alitaja majina walioteuliwa ni Mabula Magangila CCM, Joel James wa Makini, John Wambura wa Chaumma, Kaswiga Bwire wa ACT Wazalendo, Devotha Alphonce wa DP na Azaliah Erasto wa UDP.

 

Imeandikwa na John Nditi (Morogoro), John Mhala (Arusha), Frank Leonard (Iringa), Diana Deus (Bukoba), Naziah Kombo (Musoma), Heckton Chuwa (Moshi) na Kareny Masasy (Msalala).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button